MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Stephen Wasira amesisitiza na kuwahakikishia Watanzania kuwa amani itaendelea kutawala hivyo wajitokeze kwa wingi siku ya kupiga kura kutimiza haki yao ya kikatiba.
Wasira ameyasema hayo mkoani Geita alipokuwa akizungumza na viongozi wa CCM kumwombea kura mgombea urais wa CCM Dk. Samia Suluhu Hassan pamoja na wagombea ubunge na udiwani waliosimamishwa na Chama.
"Nataka kuwaambia, umoja wetu na amani yetu ndiyo msingi wa maendeleo yetu na lazima tung'ang'anie umoja.
"Nimesikia huko watu wanasema watu wasiende kupiga kura, wako kwenye mitandao wanasema wakati Watanzania wanapiga kura wao wataandamana.
"Sasa mimi nataka kuwaambia ndugu zangu wa Geita na Watanzania, tarehe 29 ni siku ya kupiga kura hakuna kuandamana wala mtoto wa maandamano, hamna, nasema hamna kwa sababu mimi ni Makamu Mwenyekiti wa Chama kinachotawala Tanzania na mpaka tarehe 29 tutakuwa bado tunatawala.
"Kwa hiyo kama alivyosema Rais (Dk. Samia Suluhu Hassan), juzi, alipokuwa anazungumza Dar es Salaam aliwaambia yeye ndiye Amirijeshi Mkuu, alikuwa hawatishi alikuwa anawaambia tu kwamba kuna serikali ambayo kazi yake ni kuhakikisha amani inakuwepo," amesema.
Amesema kuwa serikali na CCM haiwezi kuruhusu uvunjifu wa amani na kuzuia umma wa Watanzania kutumia haki ya kikatiba kuchagua viongozi.
"Wewe uje uvuruge amani sisi tunakuangalia haiwezekani, kwa hiyo nendeni muwaambie wapigakura waandamane kwenda kupiga kura hakuna mtu atawabughudhi hata mmoja, hamna.
"Hatuwezi kuruhusu watu wachache wanaotumiwa na watu wa nje kuleta fujo katika nchi yetu, hapana, tunataka wa hapa na wa nje wenye chokochoko wapate habari kwamba hatukubali na uchaguzi utafanyika tena kwa amani," amesisitiza.
