Washuhudia uwekezaji wa kisasa ikiwemo ujenzi wa Gati jipya la kupokea Meli kubwa, jengo la kisasa la mizigo na jengo la abiria._
Bandari ya Kemondo iliyopo Tarafa ya Katerero Bukoba mkoani Kagera imefanyiwa maboresho na uwekezaji mkubwa sana na Serikali ya Rais Samia na sasa ina uwezo wa kupokea meli yoyote ile duniani. Bandari hii inahudumia ukanda mzima wa Ziwa Victoria, Maziwa Makuu kwenda hadi nchi za nje.
Afisa Tarafa ya Katerero iliyopo Bukoba mkoani Ndugu Bwanku M Bwanku amewapeleka wananchi wa Kemondo na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Bujunangoma na Kashozi kushuhudia uwekezaji huu mkubwa na kuona jinsi Serikali ilivyoiboresha Bandari ya Kemondo ili iweze kuchochea uchumi wa wananchi katika usafiri na usafirishaji wa mizigo.
Toka mwaka 2024 Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imefanya maboresho makubwa na uwekezaji wa Bilioni 20 kwenye Bandari ya Kemondo kwa kujenga Gati jipya la kisasa linaloweza kupokea meli yoyote kubwa duniani, kujenga jengo la kisasa la abiria pamoja na jengo la mizigo. Kabla ya uwekezaji huu, Bandari ya Kemondo ilikua haina uwezo wa kupokea meli kubwa kwasababu ya Gati dogo na mapato yalikua chini sana. Maboresho yamekamilika yakifanywa na Mkandarasi wa Kichina Kampuni ya CRMBEG.
Sasa Bandari ya Kemondo inapokea meli yoyote ile yenye ukubwa wowote, mapato yameongezeka mara 4 kutoka mwanzo na wananchi wanafurahia kusafirisha mizigo yao na kusafiri wao wenyewe bila changamoto yoyote ile baada ya maboresho haya makubwa yaliyofanywa na Serikali ya Rais Samia.
Bandari ya Kemondo iliyopo kwenye Tarafa ya Katerero wilayani Bukoba ni moja ya Bandari kubwa 10 Tanzania na ni Bandari yenye eneo kubwa sana nchini.