Mgombea Mwenza wa nafasi ys Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi mbele ya mamia ya wananchi wa Kata Puma, Jimbo la Ikungi Magharibi Mkoani Singida, Amemnadi na Kumuombea kura Mgombea Ubunge wa Ikungi Magharibi, anayetetea nafasi yake hiyo Mhe. Elibariki Immanuel Kingu mapema leo Jumatano Oktoba 15, 2025.
Balozi Nchimbi amepokelewa na mamia ya wananchi wa Kata hiyo mapema leo asubuhi, ikiwa ni Mkoa wake wa 23 tangu kuzinduliwa kwa Kampeni za Chama Cha Mapinduzi Agosti 28, 2025 Jijini Dar Es Salaam, akisaka kura za ushindi za Mgombea Urais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kura za Wabunge na Madiwani wanaotokana na Chama Cha Mapinduzi akiwemo Mgombea Ubunge huyo Mhe. Kingu.
Wakati wa hotuba yake Mhe. Kingu ameeleza mafanikio kadhaa yaliyopatikana ndani ya Miaka minne ya Dkt. Samia madarakani, ikiwemo maboresho makubwa ya sekta ya afya, upatikanaji wa dawa muhimu na Vifaa tiba kwenye Jimbo hilo, ujenzi wa shule za msingi na sekondari, uongezaji wa madarasa kwenye shule zilizopo sambamba na uwezeshaji wa wananchi kiuchumi kupitia Mikopo ya Halmashauri na Ruzuku za mbolea, pembejeo za kilimo na chanjo kwa mifugo.
Amesisitiza pia umuhimu wa kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, 2025 ili kukipa ushindi Chama Cha Mapinduzi, akiwarai wananchi wa Jimbo hilo na Mkoa wa Singida kwa ujumla kuendelea kulinda amani na utulivu wa Tanzania kwa kuhakikisha hawarubuniwi ama kushawishiwa kujiingiza katika matendo yoyote yale yenye kuashiria Uvunjifu wa amani na usalama wa Nchi wakati wa kura na hata baada ya uchaguzi mkuu wa Tanzania.