DKT SAMIA AONGEZA VIVUTIO 69 VYA UTALII KWA MPIGO NGORONGORO


Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan imeongeza vivutio takribani 69 vya utalii kupitia Hifadhi mpya ya Kijiolojia ya Ngorongoro (Ngorongoro-Lengai Geopark).

Hayo yamebainika leo Oktoba 16, 2025, wakati Makamu wa Rais, Dkt. Phillip Isdor Mpango, alipomwakilisha Rais Samia kuzindua Makumbusho kubwa ya Hifadhi ya Jiolojia ya Ngorongoro (Ngorongoro-Lengai Geopark Museum) iliyojengwa kwa ushirikiano na Serikali za Tanzania na China kwa thamani ya TZS Bilioni 32. 

Hifadhi ya Jiolojia na Utamaduni (Geopark) ni hadhi inayotolewa na UNESCO kwa mkusanyiko wa maeneo yenye taswira maalum na maumbo ya miamba na milima, yenye mvuto wa kipekee kihistoria na kiutamaduni. 

Pamoja na Makumbusho mradi huo umehusisha majengo ya kuhifadhi nyayo za binadamu wa kale na miundombinu mingine ya uhifadhi na utalii. 


“Kwa Afrika Tanzania ni ya pili baada ya Moroko kupata hadhi hii. Vivutio hivi vipya vitasaidia kuleta watalii zaidi hapa nchini lakini na kuendeleza jamii,” alisema Dkt. Mpango. 

Hifadhi ya Jiolojia ya Ngorongoro-Lengai yenye jumla ya vivutio vya kiutalii 69 ndani yake ikiwemo Kreta au Kasoko ya Ngorongoro, Nyayo za Binadamu wa Kale, Eneo la zamadamu la Olduvai, Mlima wa Oldonyo Lengai na maeneo mengine yenye upekee wa kiutamaduni zikiwemo tamaduni kama za Wamasai, Wairaq, Wadatoga, Wahadzabe na maeneo mengine ndani na nje ya mipaka ya sasa ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, itasaidia kuongeza mazao mapya ya utalii.

“Unaweza kudhani Rais Samia katika utalii kafanya Royal Tour tuu lakini mradi huu ni ushuhuda wa kazi za mikono yake katika kila eneo la utalii,” anasema Joseph Tadano mdau wa utalii.

Post a Comment

Previous Post Next Post