Mgombea ubunge wa Jimbo la Mtumba kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Anthony Mavunde, amesema baadhi ya wananchi waliopitiwa na barabara ya kwenda jeshini katika Kata ya Kikombo wameshaanza kupokea fidia, huku akiahidi kuhakikisha wananchi wote wanapokea fidia zao.
Akizungumza wakati wa muendelezo wa kampeni zake Kata ya Kikombo, Jimbo la Mtumba, Mavunde amesema serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ipo tayari kulipa fidia hizo. Hivyo, wananchi wanapaswa kuendelea kukiamini chama na serikali, kwani wote waliopitiwa na barabara, watalipwa fidia zao.
Aidha, Mavunde amezungumzia changamoto ya muda mrefu ya upatikanaji wa maji katika eneo la Chololo Magharibi, akisema kuwa wafanyakazi wa TANESCO tayari wameshafika ili kufanya tathmini, na kiasi cha fedha kinachohitajika ni milioni 52. Swala hilo liko Wizara ya Nishati, hivyo ameahidi kufuatilia swala hilo ili kuhakikisha changamoto hiyo inatatuliwa kwa haraka.
Kwa upande wa Mtaa wa Ngh’ungugu, amesema tayari serikali imetenga shilingi milioni 23 kwa ajili ya kumalizia miradi ya ujenzi wa madarasa na kujenga nyumba za walimu, ili kuwawezesha kufanya kazi katika mazingira bora na kuwahudumia watoto wa jimbo hilo kikamilifu.
Amesema hatua hizo ni sehemu ya dhamira yake ya kuhakikisha maendeleo endelevu na maisha bora kwa wananchi wa Kata ya Kikombo na maeneo jirani, huku akihimiza wananchi kuhakikisha tarehe 29 Oktoba 2025 wanajitokeza kupiga kura kwa wagombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa nafasi ya Urais, Ubunge na Udiwani.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Ndugu Donald Mejitii, amewataka wananchi wa Jimbo la Mtumba kuhakikisha wanakipa ushindi wa kishindo Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi ujao akisisitiza kuwa chama hicho kiko tayari kuwalipa wananchi maendeleo ya kweli, endapo wataendelea kukiamini na kukipa ridhaa ya kuongoza.