Mgombea Ubunge wa Ikungi Magharibi kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM Mhe. Elibariki Kingu Ikungi Magharibi ameeleza kuwa Chama hicho kilikubaliana kwa pamoja kwa kuzingatia kanuni na taratibu za Chama hicho, kumpitisha Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea Urais wa wa Tanzania kupitia Chama hicho.
Akizungumza mbele ya Mgombea Urais huyo wakati wa Mkutano wa kampeni leo Septemba 09, 2025, Kingu ameahidi pia kumlinda na kumtetea Mgombea Urais huyo, na kuwataka watanzania kumpuu,a mwanasiasa na aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba Bw. Humphrey Polepole ambaye amekuwa akikosoa mchakato uliotumika kumpata Dkt. Samia kuwania nafasi hiyo.
Katika hatua nyingine Kingu amelitaja Jimbo la Ikungi kuwa na wapigakura wengi wa Chama Cha Mapinduzi CCM, akiwakosoa vikali wale wote wanaodai kuwa Chama hicho na Mgombea Urais wake wamekuwa wakitumia nguvu kubwa katika kujaribu kupendwa na watanzania.
"Nikuambie Mhe. Mgombea wetu kuwa watu wote hawa wamekuja kwa mapenzi yao, kuna Vikaragosi eti wanasema wewe unalazimisha kupendwa, naomba nikupe rekodi kuwa Jimbo la Ikungi Magharibi lina wapigakura 140, 000, nataka nikuambie Oktoba 29, utazoa kura mpaka ushangae. Tembea kifua mbele, tutakulinda Dkt. Samia." Amesema Mwanasiasa huyo Kijana.
Kingu pia amemshukuru Dkt. Samia kwa utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo kwenye Jimbo la Ikungi Magharibi kwa miaka yake minne ya uongozi ikiwemo huduma ya maji, umeme, afya, elimu pamoja na ukuzaji wa diplomasia ya uchumi kote duniani, akiahidi kuzisaka kura za kishindo kwa Dkt. Samia kuelekea uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
