WANANCHI MSITUPE TAKA KWENYE MITARO, HIFADHINI MIRADI YA BARABARA*:ISMAIL USSI


Wananchi ambao wanapitiwa na miradi ya Barabara wametakiwa kulinda na kuhifadhi miradi ya  Barabara  na   kuachana na dhana ya kutupa uchafu katika mitaro  ya maji inayokuwa imetengenezwa na kusababisha uchafuzi wa Barabara.

Wito huo umetolewa na Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa  ndugu Ismail Ussi wakati akiweka jiwe la Msingi katika barabara ya  Ihungo yenye urefu wa Km. 1.25 yenye thamani ya shilingi Milioni 506.4   ambayo inaunganisha kata za Kashai na Shambya  kwa kiwango cha lami inayotekelezwa na TARURA.

"Kumekuwa na tabia ya uchafuzi wa mazingira kwa barabara zinazopita karibu na makazi yenu,mtu anakusaya taka anatupa katika mitaro anasema mvua ikinyesha  itasafirisha uchafu hii haikubariki na imeharibu barabara nyingi , tutunze na kuthamini Miradi inayoletwa kwa sababu inatumia pesa nyingi sana "Amesema Ussi

Aidha, ameipongeza TARURA kwa kuendelea kung’arisha mji wa Bukoba hasa mitaa ya pembezoni kwa kuwawekea lami na taa za barabarani jambo ambalo linakuza uchumi wao  kwa kufanya biashara usiku na mchana.

Naye, Meneja wa TARURA wilaya  ya Bukoba Mhandisi Emmanuel Yohana amesema kuwa   mradi huo unatekelezwa kwa awamu tatu na lengo kuu ni kuendelea kuweka lami katika mitaa na kupendezesha mji wa Bukoba

Amesema mradi huu umefika asilimia 40 na ulianza kutekelezwa  Septemba mwaka 2024 na utakamilika Novemba 2025 ili  wananchi wa Kata ya kashai na Nshambya wanaunganishwa na barabara hiyo  waendelee kuitumia  barabara kwa urahisi  pamoja na wananchi kufanya biashara nyakati za usiku baada ya kuwekewa taa.

Post a Comment

Previous Post Next Post