MAKANDARASI KUNUFAIKA NA HATIFUNGANI YA MIUNDOMBINU YA SAMIA


Serikali kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa kushirikiana na Benki ya CRDB imeboresha Hatifungani ya  Miundombinu ya Barabara za Wilaya (Samia Infrastructure Bond) kwa lengo la kuwawezesha Makandarasi kufanya kazi kwa wakati na kwa ufasaha.

Hayo yamebainishwa na Mhasibu Mkuu wa TARURA CPA. Jacob Nyaulingo wakati wa ufunguzi wa kikao kazi kilichowakutanisha wahasibu wote wa TARURA, Wataalam kutoka Benki ya CRDB, Wawakilishi wa Mameneja wa Mikoa wa TARURA na baadhi ya Makandarasi.

CPA. Nyaulingo amebainisha kuwa lengo la serikali ni kuboresha Hatifungani ya Miundombinu ya Samia (Samia Infrastructure Bond) ili kuwawezesha Makandarasi katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa barabara za Wilaya zinazosimamiwa na TARURA. 

"Hatifungani hii imeboreshwa na kuanzia mwaka huu wa fedha 2026/2027 tunaendelea kuwasisitiza Makandarasi nchini kuchangamkia fursa hii ili kupata fedha ya kutekeleza miradi kwa wakati", amesema CPA. Nyaulingo.

Kwa upande wake, Bw. Michael Paul Meneja Mwandamizi kutoka Benki ya CRDB Kitengo cha Mikopo ametoa wito kwa Makandarasi wote nchini kuchangamkia fursa ya Samia Infrastructure Bond ili kuhakikisha miradi ya serikali inayosimamiwa na TARURA inakamilika kwa wakati kwani upatikanaji wa fedha kupitia Benki hiyo umerahisishwa na hii ni baada ya serikali kufanya maboresho katika taratibu za kuomba mikopo katika hatifungani hiyo.

"Lengo la Hatifungani hii kati ya Serikali na Benki ya CRDB ni kuhakikisha Makandarasi wanapata fedha kwa urahisi ili waweze kutekeleza miradi kwa wakati na sisi kama  Benki hili tunalitekeleza na wapo wengi wanaonufaika", amesema Bw. Michael.

Kwa upande wake, mmoja wa wanufaika wa Hatifungani hiyo kutoka kampuni ya MORCEP, Bi. Nasra Ramadhani amesema kuwa kampuni yao huchukua mikopo mara kwa mara kutoka Benki ya CRDB na hutekeleza miradi kwa wakati huku akibainisha kuwa hakuna masharti magumu katika upatikanaji wa mikopo hiyo.

"Kampuni yetu ni mnufaika mojawapo wa hii Samia Infrastructure Bond, nawashauri Makandarasi wengine kuchangamkia fursa hii kwani inasaidia sana katika utekelezaji wa miradi maana fedha hupatikana kwa wakati". Amesema Bi. Nasra.

Post a Comment

Previous Post Next Post