Wakati kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu zikifikia siku ya tatu, Mgombea Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt Samia Suluhu Hassan amesema chama chake hakina mambo mengi, kila kinachoahidi kitakitekeleza.
Kauli hiyo ya Dkt Samia inakuja ukiwa ni msimamo wa chama hicho wakati ambao, tayari alishatoa mwelekeo wa atakayoyafanya ndani ya siku 100 atakapochaguliwa kuwa Rais wa awamu ya saba wa Tanzania, katika hafla ya uzinduzi wa kampeni za urais, Oktoba 28, 2025, Dar es Salaam.
Miongoni mwa aliyoahidi kuyafanya ndani ya siku hizo, ni kuandaa mazingira ya kuanza mchakato wa Katiba Mpya, kuanza utekelezaji wa Gridi ya Taifa ya Maji, Bima ya Afya kwa Wote na kugharimia matibabu ya saratani, figo na moyo kwa Watanzania wasio na uwezo.
Ukiacha ahadi za jumla, Dkt Samia ameahidi kuirudisha Morogoro kuwa mkoa wa viwanda, huku akisisitiza kukomesha migogoro ya ardhi hasa wakulima na wafugaji, kuboresha upatikanaji wa maji safi na huduma nyingine mkoani humo.
Dkt Samia ameeleza hayo kwa nyakati tofauti, leo, Jumamosi Agosti 30, 2025 alipozungumza na wananchi wa mikoa ya Morogoro na Dodoma ikiwa ni mwendelezo wa kampeni zake za kugombea urais kupitia CCM.
Akiwa Kibaigwa, wilayani Kongwa mkoani Dodoma, Rais Dkt Samia amesema ni kawaida ya CCM kutokuwa na maneno mengi, kwani kila kinapoahidi kinatekeleza.
Ameijenga hoja hiyo akijivunia utekelezaji wa miradi mbalimbali ukiwemo wa kituo cha kupoza umeme kutoka Gairo hadi Kongwa na hivyo kuimarisha uhakika wa upatikanaji wa huduma hiyo kwa maeneo hayo.
“Serikali ya CCM haina maneno mengi, tukiahidi tunatekeleza. Nawaomba sana mkachague Chama Cha Mapinduzi, nendeni (WanaCCM) kata kwa kata, kijiji kwa kijiji, mtaa kwa mtaa, nyumba kwa nyumba, tukachague mafiga matatu,” amesema Dk Samia.
Kwa kuwa Kongwa ina wafugaji na wakulima, amesema wataanzisha minada 10 ya mifugo, majosho 35 na machinjio nne ili kuimarisha kilimo na ufugaji na kuongeza upatikanaji wa umeme katika Vitongoji vyote vya Wilaya Kongwa.
Vituo vipya vya afya 10 na Zahanati 21, amesema zitajengwa wilayani Kongwa, sambamba na ujenzi wa Hospitali ya Wilaya, huku shule mpya zikiendelea kujengwa kwa kuzingatia ongezeko la idadi ya watu.
“Ombi langu kwenu au wito wangu, ili safari ya maendeleo iendeleee kwa ufanisi, ikifika Oktoba 29, nendeni mkapige kura asibaki mtu nyumbani. Kila aliyejiandikisha akapige kura kukichagua Chama Cha Mapinduzi, kinachosema na kutenda,” amesema.
Akiwa Morogoro
Akiwa wilayani Kilosa Mkoa wa Morogoro alikoanzia ziara yake kwa siku ya leo, Dkt Samia ameahidi kuongeza maeneo ya wafugaji katika Wilaya ya Kilosa kutoka ekari milioni 3.46 hadi milioni 6 ili kumaliza migogoro ya wakulima na wafugaji.
Amesema Wilaya ya Mvomero imefanikiwa kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji kupitia programu ya ‘Tutunzane’ na kwamba atahakikisha inatekelezwa hata Kilosa.
"Tutakuja na mpango wa kuongeza maeneo ya wafugaji, tuna maeneo ya ekari milioni 3.46, tunakwenda kuongeza hadi ekari milioni 6 kwa ajili ya wafugaji. Hii ni kwa ajili ya kupunguza migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji," amesema Dkt Samia.
Ameeleza mashamba yenye ekari 53,475 ambayo yalikuwa hayajaendelezwa, yalifutwa benki zake na kupimwa ekari 21,872 ambazo ziligawiwa kwa wananchi kwa ajili ya kilimo, makazi na uwekezaji.
Ameongeza wananchi 8,557 kutoka kwenye vikindi 186 vilivyopo katika vijiji 11, walifaidika na mpango huo na sasa kazi ya kupima inaendeleo na kazi ya ugawaji wanakwenda kuimaliza wakichaguliwa kuendelea na uongozi.
"Niwahakikishie kwamba tutagawa mashamba bila kuonea mtu, bila dhuluma. Na wale wenye matatizo tunatambua, watapata vipande vya ardhi," ameeleza na kuibua shangwe kutoka kwa wananchi waliohudhuria mkutano huo.
Akizungumza na wananchi wa Jimbo la Gairo, Rais Dkt Samia amewasihi kukipigia kura chama hicho ili kiendeleze kazi kubwa iliyofanyika miaka mitano iliyopita ikiwemo utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye sekta za afya, elimu, maji na miundombinu.
Amesema akichaguliwa miaka mitano ijayo, atahakikisha Serikali inakamilisha miradi mingine ikiwemo ya barabara kutoka Robeho hadi Kisihi. Pia, ameahidi kuongeza vituo vitano vya afya katika eneo hilo.
"Tufanye kazi, Oktoba 29, 2025 tukakipigie kura Chama cha Mapinduzi. Mkamchague Rais, wabunge na madiwani wa CCM ili tukaendeleze kazi ya kuongoza dola," amesema Rais Samia.