WATANZANIA KUNUFAIKA NA HUDUMA ZA TIBA ASILI ZINAZOCHANGANYA SAYANSI NA URITHI WA ASILI


Watanzania wanatarajia kunufaika zaidi na huduma za tiba asili na tiba mbadala baada ya Serikali kuimarisha mfumo wa usimamizi, utafiti na upatikanaji wa dawa salama na zenye viwango vya kitaalamu.

Hayo yamebanishwa Agosti 29, 2025 na Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Khatibu Kazungu katika maadhimisho ya Siku ya Tiba Asili ya Mwafrika yaliyofanyika Dodoma, alipokuwa akimwakilisha   Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa. 

Dkt. Kazungu amesema wananchi sasa wanapata huduma jumuishi za tiba asili katika hospitali 14 za mikoa, hali inayowawezesha kuchagua kati ya tiba za kisasa, tiba asili au kutumia zote kwa pamoja.

“Huduma hii inamuwezesha mteja kufanyiwa vipimo vya kitaalamu na kupewa ushauri sahihi kuhusu tiba itakayomfaa. Hii inaleta faraja kubwa kwa wananchi kwani sasa tiba asili inapatikana kwa usalama zaidi ndani ya mfumo wa hospitali zetu,” amesema Dkt. Kazungu.

Dkt. Kazungu amesema Wananchi pia watanufaika na ajira mpya kutokana na kuanzishwa kwa kiwanda cha kuzalisha dawa za tiba asili cha NIMR-Mabibo, ambacho kitategemea malighafi kutoka kwa wakulima wa miti dawa. 

Aidha, amesema Serikali imeboresha usindikaji na ufungashaji wa dawa za tiba asili, na sasa zaidi ya dawa 141 zimesajiliwa huku zingine 42 zikiwa zimefanyiwa tafiti za usalama na ubora.

Kwa wananchi wanaotumia tiba asili, Dkt. Kazungu amesema hatua hizi zinamaanisha kupata huduma zilizo salama zaidi, zenye ubora unaokubalika na bei nafuu.

Amesema kwa mujibu wa Rais  Samia Suluhu Hassan, maendeleo haya ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050 inayolenga kuhakikisha Watanzania wanapata afya bora kupitia urithi wa tiba za asili na sayansi ya kisasa.

Post a Comment

Previous Post Next Post