DKT SAMIA KUMWAGA NEEMA DODOMA


Neema ya fursa ya ajira na maendeleo inanukia kwa wananchi wa Mkoa wa Dodoma, baada ya mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt Samia Suluhu Hassan kuahidi atakayoyafanya kwa miaka mitano ijayo.

Kumaliza changamoto ya maji, umeme, kuboresha huduma za kijamii na kujenga kongani za viwanda, ni miongoni mwa mambo atakayoyafanya katika Mkoa huo kwa miaka mitano ijayo ya uongozi wake, huku akiwaomba wananchi wampigie kura.

Dkt Samia ameyasema hayo leo, Jumapili Agosti 31, 2025 alipozungumza katika wilaya mbalimbali za Mkoa wa Dodoma katika mwendelezo wa kampeni zake za kusaka kura alizozianza Agosti 28, mwaka huu, jijini Dar es Salaam.

Mgombea huyo, amesema amejipanga kumaliza tatizo la maji ndani ya Mji wa Dodoma hasa ukizingatia eneo hilo ni makao makuu ya nchi.

“Dodoma ni makao makuu ya nchi, si vyema kuwa na shida ya maji. Kwa hiyo tunakwenda kumaliza kabisa shida ya maji kupitia mradi mkubwa utakaotoa maji Ziwa Victoria hadi haoa Dodoma,” amesema.

Katika kumaliza tatizo hilo, amesema atakamilisha ujenzi wa bwawa la Fakwa ambalo nalo litasaidia kupeleka maji katika jiji hilo.

Dkt Samia amesema Serikali yake itamaliza tatizo la umeme jijini humo, kwa kukamilisha utekelezaji wa mradi wa njia ya kusafirisha nishati hiyo kutoka Chalinze hadi Dodoma kilovoti 400.

“Umeme wakati mwingine mdogo, lakini unakatika. Tunataka Dodoma iwe ya viwanda na kazi zote zisisite kwa sababu ya umeme,” amesema.

Amesema ndani ya jiji hilo, atakamilisha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato kabla ya mwaka 2027.

Kumaliza migogoro ya ardhi ni jambo lingine, alilosema atahakikisha linakamilishwa katika jiji hilo, kwa kuongeza kasi ya upimaji na usajili wa ardhi.

“Tunakwenda kuongeza kasi ya upimaji na usajili wa ardhi ili kumaliza migogoro na Ndejembi (Deogratius) ndiye mwenye wadhifa huu, sasa sijajua ataendelea nao au nitampanga mwingine sijajua bado,” amesema.

Dkt Samia amesema Serikali yake itakamilisha ujenzi wa uwanja mkubwa wa mpira wa miguu na tayari mkandarasi ameshapatikana.

“Mkandarasi amepatikana tukimaliza pilika hizi, tumeshamkabidhi kazi, tukimaliza pilika hizi tunakwenda kuanza kazi,” amesema.

Amesema atavutia uwekezaji hasa kwenye viwanda na uongezaji wa thamani kwa mazao yanayopatikana katika mkoa huo.

“Tumeanzisha kilimo cha mashamba makubwa cha wenzetu wa Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT), wamelima mazao tumeanza kuyaona, kinachofuata ni kuanza kuwawekea viwanda vya kuongeza thamani,” amesema.

Dkt Samia amesema Serikali yake itakuza uwezo wa ndani katika kutekeleza vipaumbele vya maendeleo na uwezekano wa kufanya hivyo utafikiwa iwapo kazi zitafanywa kwa bidii, weledi na maarifa na kukusanya fedha za ndani.

“Niwaombe ndugu zangu na nadhani sina haja ya kuwaomba sana hasa kwa sababu mlishasema kazi imemalizika mnasubiri Oktoba 29, mkatiki tumalize mchezo,” amesema.


Afurahia mapokezi Dodoma

Katika hotuba yake, Dkt Samia ameelezea kufurahishwa na mapokezi aliyopata kwa wananchi wa Mkoa wa Dodoma walioanza kujitokeza kwa wingi kuanza jana katika mkutano wa hadhara wa Kibaigwa wilayani Kongwa.

“Toka nimeingia jana pale Kibaigwa, leo Chemba, Kondoa hapa Dodoma Manispaa, Dodoma mmefunika.Dodoma CCM ina wenyewe na wenyewe ndio nyinyi hapa (wanachama wa CCM).

“Wale wenye maswali, nadhani kidogo…wanaanza kufuta, wale wenye kuhoji wanaanza kufuta. Kwa umma huu, CCM oyee, nawashukuru sana ndugu zangu WanaDodoma kwa hamasa na mapokezi makubwa, mmethibitisha hapa ndio makao makuu ya Chama Cha Mapinduzi,” amesema Dkt Samia.

Leo Agosti 31, Dkt Samia alifanya mikutano ya hadhara ya kuwanadi na kuwaombea kura madiwani na wabunge wa majimbo ya Chemba, Kondoa Mjini na Vijijini,pamoja na Dodoma Mjini.

Katika mikutano hiyo, Dkt Samia aliwaomba wananchi Dodoma na Watanzania kuendelea kukiamini Chama Cha Mapinduzi kwa ndicho kinatekeleza mambo kwa uhakika zaidi na siyo ‘tonetone’.

Post a Comment

Previous Post Next Post