Chama cha Mawakili Zanzibar ZLC imeahidi kuendeleza ushirikiano na serikali, Mahakama na wadau wengine wa sheria katika kuhakikisha dhamira ya serikali ya Kuifanya kampeni ya Kitaifa ya msaada wa kisheria ya Mama Samia inakuwa endelevu kwani ndicho kiini cha utekelezaji wa utawala wa sheria na haki za binadamu nchini.
Mbele ya Mgeni rasmi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi, wakati wa uzinduzi wa kampeni ya msaada wa kisheria mkoa wa Kusini Unguja leo Mei 10, 2025, Rais wa ZLS Wakili Joseph Magazi amepongeza pia jitihada zinazochukuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan na Rais Dkt. Mwinyi katika kuhakikisha kuwa huduma hiyo ya kisheria inamfikia kila mwananchi.
Aidha ameshauri pia kutathimini uendelevu wa kampeni hiyo, wakipendekeza kuwe na mfumo madhubuti wa ufuatilia wa mashauri yanayoanzishwa wakati wa utekelezaji wa kampeni hiyo visiwani Zanzibar ili kuendelea kutoa msaada hata pale kampeni hiyo itakapokuwa imemalizika kwenye maeneo mbalimbali.
"Tunatambua kuwa kampeni hii ina muda maalum hivyo basi ni muhimu kuwa na mpango wa kuhakikisha kuwa msaada huu wa kisheria unaendelea pindi kampeni itakapokamilika. ZLC ipo tayari kwa kushirikiana na serikali kuandaa mkakati wa pamoja katika kuendelea kuihudumia jamii." Amesema.
Kadhalika ametoa rai ya kuongezwa kwa rasilimali fedha kwa idara ya msaada wa kisheria visiwani Zanzibar ili kuendelea kukuza ufanisi wa utoaji wa huduma, kupunguza mrundikank wa mashauri pamoja na kuongeza wigo wa ufikiaji wananchi hasa maeneo ya Vijijini pamoja na kuandaa mfumo wa pamoja utakaowezesha watoa huduma za msaada wa kisheria ikiwemo asasi za kiraia kufanya kazi kwa kushirikiana katika kushughulilia mashauri kwa mtazamo wa pamoja.