Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania, UWT Taifa Mary Pius Chatanda amesema Kampeni ya Kitaifa ya Msaada wa kisheria ya Mama Samia inayotekelezwa nchi nzima imekuwa msaada mkubwa kwa wanawake ambao wamekuwa wakisumbuliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya mirathi.
Chatanda amesema hayo leo Mei 10, 2025 wakati wa uzinduzi wa Kampeni hiyo kwenye Kijiji cha Mtende mbele ya mgeni rasmi wa uzinduzi huo Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi ambapo amebainisha kuwa awali wanawake wengi walikuwa hawana pa kwenda na wakidhulumiwa haki zao lakini tangu kuanza kutekelezwa kwa kampeni hiyo, wanawake wengi wamepata haki zao.
"Nimshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan na wewe Mwenyewe kwa kuanzisha jambo hili la kutoa huduma za msaada wa kisheria, jambo hili wanufaika wakubwa ni sisi wanawake kwasababu wanawake tumekuwa na matatizo mengi, hatuna pa kukimbilia na hatuna uwezo wa kupata Mawakili kutusaidia lakini tokea mmeanzisha huu utaratibu akinamama wengi wameenda kutoa shida zao, wamesikilizwa na wamesaidiwa hasa katika masuala ya ardhi.", ameeleza.
Chatanda katika salamu zake amemuomba Rais Samia na Rais Mwinyi kuhakikisha kuwa kampeni hii inakuwa endelevu na iwafikie wengi zaidi kwani wananchi wengi hususan wanawake wamekuwa wakipitia changamoto mbalimbali za kisheria huku wakiwa hawana uwezo wa kugharamia huduma hizo Mahakamani na kupata Mawakili wa kuwasimamia