Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, amesema mazungumzo kati ya Tanzania na Finland yamejikita katika kuimarisha ushirikiano kwenye maeneo ya pamoja ya maendeleo, huku nchi hizo zikiweka wazi dhamira ya kuendeleza ushirikiano wa karibu zaidi kwa manufaa ya wananchi wao.
Akizungumza baada ya mazungumzo hayo, Rais Samia alisema maeneo yaliyogusiwa ni pamoja na sekta ya misitu, biashara, uwekezaji, madini, utalii, elimu, uwezeshaji wa wanawake, TEHAMA na uhamasishaji wa teknolojia.
“Ni maeneo ambayo kwa muda mrefu tumekuwa tukiyashughulikia kwa pamoja na wabia wetu wa maendeleo, na tumekubaliana kwamba bado kuna fursa kubwa ya kukuza ushirikiano zaidi katika maeneo haya,” alisema Rais Samia.
Katika kuonyesha kuimarika kwa mahusiano hayo, Rais Samia alieleza kufurahishwa kwake na hatua ya Rais wa Finland, Alexander Stubb, kuzindua rasmi Mpango wa Forland, unaolenga kuzijengea uwezo taasisi za mafunzo katika sekta ya misitu nchini.
“Katika ziara hii, nafurahi kwamba Rais Stubb mwenyewe atazindua Mpango wa Forland unaolenga kuzijengea uwezo zaidi taasisi za mafunzo kwenye sekta ya misitu nchini,” alisema Rais Samia.