Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa wamekubaliana na Rais wa Finland Mhe. Alexander Stubb kushirikiana kwa pamoja katika kutimiza adhma ya Serikali ya Tanzania ya kufikia asilimia 80 ya matumizi ya nishati safi nchini Tanzania kufikia mwaka 2034.
Rais Dkt. Samia amebainisha hayo mbele ya wanahabari leo Jumatano Mei 14, 2025 Ikulu ya Dar Es salaam mara baada ya mazungumzo yake na Rais Stubb aliyewasili nchini Tanzania leo kwa ziara ya kikazi, kwa mualiko wa Rais Samia ikiwa ni Miaka 22 imepita tangu Mhe. Stubb kufika Tanzania wakati akiwa Waziri wa Biashara.
Aidha Rais Samia amebainisha kuwa katika mazungumzo yao ameeleza kuwa amezikaribisha sekta binafsi nchini Finland kushirikiana na serikali ya Tanzania katika mkakati wake wa uongezaji wa thamani kwenye madini, ili kuhakikisha madini hayo yanaongezwa thamani kabla ya kusafirishwa kwenda nje ya nchi.
Katika mazungumzo yao pia, Rais Samia na Rais Stubb, wamekubaliana kushirikiana kwenye sekta ya Utalii ili kuongeza idadi ya watalii wa Finland. wanaofika nchini kutalii kutoka 5067 waliofika kutalii nchini Mwaka 2024, wakikubaliana pia kushirikiana kwenye maeneo mapya ya uchumi wa buluu, nishati, elimu pamoja na mahusiano ya kisiasa ili kuwa na uhusiano wa Kibunge.
Katika hatua nyingine Rais Samia pia ameiomba Finland kuendelea na kuimarisha ushirikiano wake katika sekta ya elimu, ikiwemo katika masomo ya ufundi stadi, mafunzo ya kidigitali, kukuza uwezo wa waalimu pamoja na kukuza ujuzi na kubadilishana uzoefu na masomo ya TEHAMA.