Tanzania imeendelea kuimarisha nafasi yake kimataifa baada ya Benki ya Dunia (World Bank – WB) kuitaja kuwa miongoni mwa nchi zilizo na ukomavu wa juu wa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika sekta ya umma.
Kwa mujibu wa Ripoti ya GovTech Maturity Index (GTMI) ya mwaka 2025, Tanzania imeorodheshwa katika Kundi A la nchi zenye ukomavu wa juu wa matumizi ya TEHAMA serikalini, kundi linalojumuisha mataifa yanayoongoza duniani katika matumizi ya teknolojia kuboresha utoaji wa huduma za serikali na ushirikishwaji wa wananchi.
Ripoti hiyo ya Benki ya Dunia imebainisha kuwa mafanikio ya Tanzania yametokana na uwepo wa mifumo madhubuti ya kidijitali ikiwemo mifumo ya msingi ya serikali, utoaji wa huduma mtandaoni, ushirikishwaji wa wananchi kidijitali pamoja na mazingira wezeshi ya sera na sheria za Serikali Mtandao.
Hii ni mara ya pili kwa Tanzania kutambuliwa kimataifa katika ripoti hiyo, baada ya mwaka 2022 kupanda kutoka nafasi ya 90 mwaka 2021 hadi nafasi ya 26 kati ya nchi 198 zilizofanyiwa tathmini, na kuingia rasmi katika Kundi A. Barani Afrika, Tanzania ilishika nafasi ya pili baada ya Mauritius na kuwa kinara wa ukanda wa Afrika Mashariki.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa mifumo ya msingi ya Serikali kama vile Mfumo wa Taarifa za Watumishi na Mishahara (HCIMS), Ajira Portal pamoja na Mfumo Mkuu wa Ubadilishanaji Taarifa Serikalini (GovESB) imechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma, kupunguza urudufu wa taarifa na kuimarisha uwajibikaji.
Katika eneo la ushirikishwaji wa wananchi, Benki ya Dunia imetaja Mfumo wa e-Mrejesho kuwa nyenzo muhimu inayowawezesha wananchi kutoa maoni, malalamiko na ushauri, jambo lililoongeza uwazi na kuimarisha imani ya wananchi kwa Serikali.
Akizungumza kuhusu mafanikio hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), Mhandisi Benedict Ndomba, amesema matokeo ya ripoti hiyo ni uthibitisho wa mwelekeo sahihi wa taifa katika kujenga Serikali ya kidijitali.
Ndomba amesema utafiti huo ulifanyika kwa takribani mwaka mmoja kwa kukusanya ushahidi wa matumizi ya TEHAMA serikalini katika nchi mbalimbali duniani, huku akizitaka taasisi za umma kuendelea kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya Serikali Mtandao katika utekelezaji wa miradi ya TEHAMA.
Mafanikio haya yanaendelea kuiweka Tanzania katika ramani ya kimataifa kama kinara wa mageuzi ya kidijitali barani Afrika na kuimarisha msingi wa kuboresha utoaji wa huduma za umma kwa maendeleo endelevu ya taifa.
