WIZARA YA MAJI YAOMBA KUIDHINISHWA BAJETI YA TRILIONI 1.016 KWA MWAKA 2025/26


Wizara ya Maji nchini Tanzania imeliomba Bunge la Tanzania kuidhinisha Jumla ya Shilingi Trilioni moja, bilioni kumi na sita, Milioni nane tisini na nne, laki tisa hamsini na nane elfu (1,016,894,958,000) kwaajili ya matumizi ya Wizara ya Maji kwa mwaka ujao wa fedha wa  2025/26.

Akiwasilisha makadirio ya Bajeti hiyo na Vipaumbele vyake Bungeni Jijini Dodoma leo alhamisi Mei 07, 2025, Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso ameliambia Bunge kuwa mpango huo wa bajeti umezingatoa kuimarisha usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji pamoja na ubora wa maji na kutekeleza jumla ya miradi 1,544 ya majisafi na usafi wa mazingira ambapo miradi 1,318 ni ya Vijijini na 226 ni ya Mijini.

Akieleza kuhusu vipaumbele kwa mwaka ujao wa fedha, amebainisha kuwa wataendelea kuimarisha uhifadhi na utunzaji wa vyanzo vya maji pamoja na uendelezaji wa vyanzo hivyo ikiwemo uchimbaji wa visima na ujenzi wa miundombinu ya uvunaji wa maji ya mvua.

Aidha wizara pia imeahidi kukamilisha mpango kabambe wa Taifa wa maji, kuimarisha usimamizi na udhibiti wa ubora wa maji kwa kuhakikisha yanakidhi viwango pamoja na kuendelea kuimarisha utoaji wa huduma endelevu pamoja na kudhibiti upotevu wa maji na kuongeza ubunifu katika utafutaji wa vyanzo mbadala vua fedha katika kuimarisha mfuko wa Taifa wa maji.

Waziri Aweso kadhalika ameeleza kuwa Kwa mwaka 2025/26 Wizara itatekeleza miradi ya gridi ya Taifa ya maji ikiwemo kutoa maji ziwa Viktoria kwenda Miji ya Dodoma na Singida, mradi wa kutoa maji ziwa Tanganyika kwenda Kigoma, Katavi na Rukwa, mradi wa kutoa maji Mto Ruvuma kwenda Mtwara na Lindi pamoja na mradi wa kutoa maji Mto Rufiji kwenda kwenye Mikoa ya Pwani na Dar Es salaam na kutoa maji Maziwa ya Viktoria na Nyasa kwenda maeneo mbalimbali ikiwemo Vijiji vya jirani na maziwa hayo.

Post a Comment

Previous Post Next Post