Waziri wa Maji Jumaa Aweso ameeleza kuwa serikali ya awamu ya sita kupitia maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan imeanza utekelezaji wa maagizo ya kuwekeza kwenye kutumika kwa dira za maji za malipo ya kabla ya matumizi kwa wananchi, katika jitihada za kuondokana na malalamiko ya wananchi kwenye ankara za maji na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa maduhuli yanayotokana na sekta ya maji.
Akiwasilisha Hotuba ya Bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka ujao wa fedha 2025/26 leo Alhamisi Mei 07, 2025 Bungeni Jijini Dodoma, Mhe. Aweso amebainisha kuwa Ufungaji wa dira hizo za maji umeanza vyema kwenye maeneo mbalimbali, akiitaja Iringa kuwa miongoni mwa maeneo yaliyoonesha mafanikio makubwa.
"Mhe. spika ni haki ya mwananchi kupata huduma ya maji safi na salama lakini maelekezo ya Mhe. Rais, maelekezo ya Bunge lako tukufu ni dhambi kubwa sana kumbambikia mwananchi bili ya maji. Mhe. Spika maelekezo ya Bunge lako na ya Mhe. Rais kwamba wizara ya maji sasa tuwekeze kwenye mita za kulipia kabla ya kutumia ili kuondokana na malalamiko ambayo hayana ulazima. Hiyo kazi tumeianza katika maeneo mbalimbali na Iringa tumefanya vizuri, ni mfano mzuri na kwa mwanzo huu tuliouanza tuna imani tutaenda kufanya kazi nzuri." Amesema Mhe. Aweso.
Akizungumzia mafanikio mengine yaliyopatikana, Waziri Jumaa Aweso amebainisha kuwa kuboreshwa kwa mifumo ya TEHAMA kwenye Wizara hiyo kumekuza uwazi na uwajibikaji katika makusanyo na matumizi ya maduhuli yatokanayo na huduma za maji sambamba na udhibiti wa upotevu wa maji.
Katika hatua nyingine amemshukuru pia Rais Samia kwa maboresho makubwa yaliyofanyika kwenye mazingira ya kazi ya watumishi wa wizara hiyo ikiwemo kukamilkma kwa ujenzi wa ofisi ya wizara ya maji na baadhi ya taasisi zake, kununuliwa kwa vitendeakazi ikiwemo vyombo vya usafiri, magari ya majitaka, mashine za utafiti wa maji chini ya ardhi pamoja na seti za mitambk ya uchimbaji visima na ujenzi wa Mabwawa.