Waziri wa Maji Jumaa Aweso amesema zaidi ya Shilingi trilioni 4 zimewekezwa katika sekta ya maji tangu Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani, akibainisha kuwa mafanikio yaliyopatikana ni matokeo ya dhamira ya dhati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye alimtaja kama nahodha, rubani na dereva wa mageuzi ya sekta hiyo.
Akiwasilisha Bajeti ya Mageuzi ya Sekta ya Maji kwa mwaka wa fedha 2025/26 bungeni jijini Dodoma, Alhamisi, Mei 8, 2025, Waziri Aweso ameeleza mafanikio makubwa yaliyopatikana katika maeneo mbalimbali, ikiwemo ongezeko la udahili katika Chuo cha Maji kutoka wanafunzi 2,320 hadi 4,260, sawa na ongezeko la asilimia 84, uanzishwaji wa Consultancy Bureau kusaidia vijana wanaohitimu na wastaafu wa sekta ya maji kwa mafunzo ya kitaalamu na ushauri wa kitaalam, tafiti na machapisho 52 ya kisayansi yaliyochapishwa na chuo hicho.
Mafanikio mengine ni Mfuko wa Taifa wa Maji kupata Dola za Marekani milioni 9.3 kwa ajili ya miradi ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, pamoja na kutoa mikopo ya riba nafuu kwa mamlaka za maji nchini.
Aidha, vyanzo vilivyotangazwa kuwa maeneo tengefu vimeongezeka kutoka 18 mwaka 2021 hadi 68, zaidi ya miti rafiki wa maji 3,715,838 imepandwa kupitia mipango ya uhifadhi wa vidakio vya maji.
Kwa upande wa ubora wa maji, Waziri alieleza kuwa Maabara ya maji ya Manyara imejengwa, na kufanya jumla ya maabara kuwa 17. Maabara 6 zikiwemo Singida, Shinyanga, Kigoma, Bukoba, Musoma na Dar es Salaam zimepata ithibati, na kufanya idadi ya maabara zinazozalisha takwimu zinazokubalika kimataifa kufikia 7 kutoka moja mwaka 2021.
Waziri Aweso amempongeza Rais Samia kwa mchango wake mkubwa na kusema:
“Kwa mapinduzi haya ya Mheshimiwa Rais, sisi Wizara ya Maji hatumdai, yeye ndiye anayetudai. Na sisi hatutachoka kumwombea. Kama Sekta ya Maji ni meli, Dkt. Samia ni Nahodha; kama ni Airbus, yeye ni Rubani; kama ni SGR ya mwendokasi, yeye ni Dereva.”