Mbunge wa Muleba Kaskazini kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM Mhe. Charles Mwijage ametoa pongezi kwa Wizara ya Maji inayoongozwa na Waziri Jumaa Aweso na watendaji wake kwa kufanikisha utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2020/25 akiwataka Wabunge kutembea kifua mbele kutokana na wingi wa miradi ya maji iliyofika kwenye maeneo yao.
"Mhe. Spika tunaenda kufikia malengo yetu na tumefikia malengo yetu yaliyoainishwa kwenye Ilani ya asilimia 85 na asilimia 95 kwenye maji Vijijini na mijini kabla ya wakati kwahiyo auau wote tuliomo humu tumeshiriki kikamilifu kwahiyo tuna uhakika wa kwenda na Pointi mkononi kabla hata ligi haijaanza." Amesema Mhe. Mwijage.
Wakati wa Mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Maji kwa mwaka 2025/26 leo Alhamisi Mei 07, 2025, Bungeni Dodoma, Mhe. Mwijage pia amepongeza utashi wa kisiasa wa Rais Samia Suluhu Hassan katika kuisimamia Wizara hiyo, akieleza kuwa ongezeko la bajeti kutoka Bilioni 600 hadi zaidi ya Trilioni moja ni mafanikio makubwa katika kutoa hakikisho la huduma ya majisafi na salama nchini.
Ameipongeza Wizara ya Maji pia kwa kuanza utekelezaji wa ushauri wa bunge na Maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwa na Gridi ya Taifa ya Maji, sambamba na ujenzi wa miundombinu mingi ya usambazaji wa maji kwenye maeneo ya Vijijini na Mijini kama sehemu ya utekelezaji wa huduma ya usambazaji wa maji nchini.
Awali wakati wa Hotuba yake, Waziri wa Maji Jumaa Aweso alibainisha kuwa miongoni mwa vipaumbele vya Wizara hiyo kwa mwaka 2025/26 ni pamoja na kutekeleza miradi ya gridi ya taifa ya maji ikiwemo mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria kwenda miji ya Dodoma na Singida; mradi wa kutoa maji Ziwa Tanganyika kwenda Kigoma, Katavi na Rukwa; mradi wa kutoa maji Mto Ruvuma kwenda Mtwara na Lindi; mradi wa kutoa maji Mto Rufiji kwenda mikoa ya Dar es Salaam na Pwani; na miradi ya kutoa maji maziwa ya Victoria na Nyasa kwenda maeneo mbalimbali ikiwemo vijiji vilivyo jirani na maziwa hayo.