DKT. BITEKO ATAJA VIHATARISHI UTEKELEZAJI WA DIRA YA TAIFA.


Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko amesema Mabadiliko ya tabianchi na kubadilika kwa siasa za dunia ni vihatarishi vinavyoweza kukwamisha kufikiwa kikamilifu kwa dira ya maendeleo ya Taifa na hivyo kutaka mpango mkakati wa kukabiliana na hatari zilizopo.


Akizungumza na wananchi wa Kanda ya ziwa wakati wa kuzindua taarifa ya maendeleo ya watu ya mwaka 2024 na Kongamano la kukusanya maoni ya dira ya Maendeleo 2050, Naibu Waziri Mkuu ametaja pia vihatarishi vingine kuwa ni mabadiliko ya tabianchi, demografia na mabadiliko ya teknolojia yanayotokea kote duniani.


Kufuatia vihatarishi hivyo, Naibu waziri Mkuu amewataka wananchi kutoa maoni yao kikamilifu kwa kuzingatia hatari hizo zilizopo duniani na kuja na mpango mzuri wa udhibiti wa hatari hizo ambazo zimekuwa zikikwamisha maendeleo ya nchi nyingi duniani hasa  zinazoendelea.


Naibu Waziri Mkuu pia amewataka washiriki wa kongamano hilo la utoaji wa maoni ya dira ya maendeleo 2050 kutafakari kuhusu aina ya Mtanzania na jamii tuitakayo miaka 25 ijayo, akisisitiza kuwa suala hilo ndilo litakalosaidia nchi kupiga hatua za kimaendeleo na kuwa na ustawi bora.


Akizungumzia faida ya ushirikishwa wa wananchi kwenye kutoa maoni yao ya dira ya maendeleo ya mwaka 2050, Dkt. Biteko amesema mchakato huo utasaidia kujenga umoja wa kitaifa na makubaliano ya pamoja kuhusu vipaumbele vinavyohitajika na wananchi wote wa Tanzania.

Post a Comment

Previous Post Next Post