BANDARI YA MBAMBA BAY KUWA KITOVU CHA BIASHARA UKANDA WA ZIWA NYASA - PROF. MBARAWA


Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mnyaa Mbarawa, amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya kimkakati ili kukuza uchumi, biashara na utalii, huku akiwataka Watanzania, hususan vijana, kuendelea kudumisha amani na kutumia fursa za ajira zinazotokana na miradi ya maendeleo. 

Amesema hayo Jumamosi Julai 11, 2026 alipowahutubia wananchi wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Bandari ya Mbamba Bay, wilayani Nyasa, mkoani Ruvuma.

Prof. Mbarawa amesema Bandari ya Mbamba Bay ni mradi wa kimkakati wa Taifa unaounganisha Tanzania na nchi jirani kupitia Ziwa Nyasa na kufungua fursa mpya za biashara, uwekezaji na ajira. 

Amebainisha kuwa mradi huo wenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 75.8 umefikia asilimia 60 ya utekelezaji na unahusisha ujenzi wa gati la kisasa, jengo la abiria, ghala la mizigo, yadi ya kuhifadhi mizigo pamoja na miundombinu mingine muhimu.

Sambamba ha hayo, ameelekeza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Mhandisi Mshauri na Mkandarasi kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati, kwa ubora na kwa kuzingatia thamani ya fedha za umma ili wananchi waanze kunufaika na huduma zinazotarajiwa.

Waziri huyo wa Uchukuzi pia amesema kuwa, Serikali kupitia Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO) inaendelea kuimarisha usafiri wa majini katika Ziwa Nyasa, huku Meli ya MV Njombe ikitarajiwa kuanza kusafirisha makaa ya mawe kutoka Mbamba Bay kwenda Monkey Bay nchini Malawi.

 Aidha, amesema Serikali imetenga Sh bilioni 3 kwa ukarabati wa meli ya MV Songea na Sh bilioni 1.25 kupitia TASAC kwa ununuzi wa boti ya uokozi na kuimarisha usalama majini.

Pof. Mbarawa ameendelea kwa kusema kuwa, kukamilika kwa Bandari ya Mbamba Bay, pamoja na maboresho ya barabara inayounganisha bandari hiyo na Bandari ya Mtwara na mpango wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Mtwara hadi Mbamba Bay, kutaimarisha ushoroba wa kusini na kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa watu na mizigo, hivyo kuchochea biashara, uwekezaji na utalii katika ukanda huo.

Akizungumza kuhusu mshikamano wa Taifa, Prof. Mbarawa amewataka Watanzania kuendelea kudumisha amani na utulivu, akisisitiza kuwa mazingira ya amani ndiyo msingi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo na ukuaji wa uchumi. 

Katika hatua nyingine, Amewahimiza vijana kutumia fursa za ajira na shughuli za kiuchumi zinazozalishwa na mradi huo badala ya kujihusisha na vitendo vinavyoweza kuhatarisha maendeleo ya Taifa.

Amesema Serikali itaendelea kuboresha maisha ya Watanzania kupitia uwekezaji katika miradi mikubwa ya maendeleo, huku akiwataka wananchi kushirikiana kulinda miundombinu ya umma ili iweze kutoa manufaa ya kudumu kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Post a Comment

Previous Post Next Post