WAZIRI PROF. MBARAWA AFUNGUA JENGO LA MUDA LA ABIRIA UWANJA WA NDEGE SONGEA,ATOA DIRA YA UBORESHAJI USAFIRI WA ANGA NCHINI


Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa (Mb), amefungua rasmi Jengo la Muda la Abiria katika Kiwanja cha Ndege cha Songea, Mkoa wa Ruvuma, lenye uwezo wa kuhudumia takribani abiria 300 kwa wakati mmoja.

Akizungumza katika hafla ya ufunguzi huo leo Julai 10, 2026, Prof. Mbarawa amesema ujenzi wa jengo hilo ni sehemu ya jitihada za Serikali kuboresha huduma za usafiri wa anga na kukidhi ongezeko la mahitaji ya abiria.

Ameeleza kuwa Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika miundombinu ya usafiri, ikiwemo viwanja vya ndege, kwa lengo la kukuza uchumi, kuongeza ushindani wa nchi na kuboresha huduma kwa wananchi.

Amesema Serikali imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi na uboreshaji wa viwanja vya ndege nchini, ikiwemo Msalato-Dodoma, Tanga, Kigoma, Tabora, Shinyanga, Lake Manyara na Sumbawanga, huku maboresho ya awamu ya kwanza yakikamilishwa katika viwanja vya Iringa, Mtwara na Songea.

Kwa mujibu wa Waziri Mbarawa, maboresho yaliyofanyika katika Uwanja wa Ndege wa Songea yamehusisha ukarabati na upanuzi wa njia ya kurukia na kutua ndege, maeneo ya maegesho ya ndege, ufungaji wa taa za kuongozea ndege, vifaa vya kisasa vya mawasiliano ya anga pamoja na miundombinu ya usalama.

Ameendelea kwa kusema kuwa, jengo hilo la muda litakuwa suluhisho wakati Serikali ikiendelea na maandalizi ya ujenzi wa jengo kubwa na la kisasa zaidi la abiria katika kiwanja hicho.

Katika hatua nyingine Prof. Mbarawa amewataka wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kushirikiana na Serikali katika kulinda na kutunza miundombinu ya kiwanja hicho ili iweze kuendelea kutoa huduma kwa Watanzania kwa muda mrefu.

Vilevile amesisitiza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kuweka kipaumbele katika uboreshaji wa miundombinu ya usafiri ili kuchochea biashara, uwekezaji na maendeleo ya kiuchumi nchini.

Aidha, Waziri Profesa Mbarawa amesema uboreshaji wa uwanja wa ndege wa Songea ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuimarisha mtandao wa usafiri wa anga nchini na kuufanya uwanja huo kuwa kichocheo cha ukuaji wa shughuli za kiuchumi, utalii na uwekezaji katika Mkoa wa Ruvuma na maeneo ya Kusini mwa Tanzania.

Post a Comment

Previous Post Next Post