WAZIRI MBARAWA AZINDUA DARAJA LA MITOMONI, ASEMA LITARAHISISHA USAFIRI RUVUMA


Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mnyaa Mbarawa, amezindua rasmi Daraja la Mitomoni pamoja na barabara zake za maingilio zenye urefu wa kilomita 8.8, akisema mradi huo utaondoa changamoto ya usafiri iliyokuwa ikiathiri wananchi wa Wilaya za Songea na Nyasa mkoani Ruvuma.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi iliyofanyika Julai 12, 2026, Profesa Mbarawa amesema daraja hilo limejengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 9.29 kupitia ushirikiano wa Serikali na Benki ya Dunia chini ya Mpango wa CERC.

Amesema kwa muda mrefu wananchi walilazimika kuvuka Mto Mitomoni kwa kutumia boti za injini na zisizo za injini, hali iliyokuwa ikihatarisha usalama wa maisha, kuchelewesha shughuli za kiuchumi na kuongeza gharama za usafiri.

“Kukamilika kwa daraja hili kunafuta changamoto hizo na kufungua fursa mpya za maendeleo kwa wananchi wa maeneo haya,” alisema Profesa Mbarawa.

Daraja hilo lina urefu wa mita 45 na upana wa mita 11.85, likiwa na njia mbili za magari pamoja na njia maalumu za waenda kwa miguu. Mradi huo pia umehusisha ujenzi wa barabara za maingilio kwa kiwango cha changarawe, makalavati, mifereji ya maji na miundombinu mingine ya kuhifadhi ubora wa barabara.

Profesa Mbarawa ameendee mradi huo utarahisisha usafirishaji wa mazao kwenda masokoni, kupunguza muda wa safari na gharama za usafirishaji, pamoja na kuboresha upatikanaji wa huduma za elimu na afya.

Ameongeza kwa kusema kuwa, utekelezaji wa mradi huo umechangia kuongeza ajira kwa wananchi wa maeneo jirani, ambapo takribani asilimia 90 ya wafanyakazi waliohusika walitoka katika vijiji vinavyozunguka mradi huo.

Katika hatua nyingine, Waziri huyo wa Uchukuzi amewapongeza TANROADS, TANROADS Engineering Consulting Unit (TECU), Mkandarasi Ovans Construction Limited pamoja na wadau wote waliofanikisha utekelezaji wa mradi huo.

Amewataka wananchi kuendelea kulinda daraja na barabara hizo kwa kuzingatia sheria za usalama barabarani na kuepuka vitendo vinavyoweza kuharibu miundombinu hiyo.

“Serikali itaendelea kuwekeza katika miradi ya maendeleo yenye lengo la kuboresha maisha ya Watanzania na kuimarisha uchumi wa Taifa,” alisema 

Post a Comment

Previous Post Next Post