WAZIRI wa Uchukuzi, Prof. Makame Mnyaa Mbarawa, amesema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia nchini ili kuongeza ufanisi katika sekta ya elimu, huku akiwataka wanafunzi kutumia fursa zinazotolewa na Serikali kufanya vizuri katika masomo na kudumisha uzalendo.
Prof. Mbarawa amesema hayo wakati wa hafla ya kukabidhi gari kwa Shule ya Sekondari ya Dkt. Samia iliyopo Wilaya ya Namtumbo, mkoani Ruvuma, kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Amesema gari hilo ni utekelezaji wa ahadi iliyotolewa na Rais Samia baada ya kupokea ombi kutoka kwa viongozi wa wanafunzi wakati wa ziara yake wilayani Namtumbo Septemba 29, 2024, hatua inayodhihirisha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuendelea kuwekeza katika elimu.
Prof. Mbarawa ameeleza kuwa gari hilo litasaidia kurahisisha shughuli mbalimbali za shule, ikiwemo usafiri wa kiutawala, ufuatiliaji wa shughuli za elimu, huduma za dharura na majukumu mengine yanayohitaji usafiri wa uhakika, hivyo kuongeza ufanisi wa utendaji wa shule.
Aidha, ameutaka uongozi wa shule kulitunza gari hilo kwa kuhakikisha linatumika kwa madhumuni yaliyokusudiwa na linafanyiwa matengenezo kwa wakati ili liendelee kuhudumia kizazi cha sasa na kijacho.
Vilevile, amewahimiza wanafunzi kuongeza bidii katika masomo, kuzingatia nidhamu na kuwa wazalendo, akieleza kuwa mafanikio yao yatakuwa njia bora ya kuthamini uwekezaji unaofanywa na Serikali katika sekta ya elimu.
Katika hafla hiyo, Prof. Mbarawa amekabidhi rasmi gari hilo kwa uongozi wa Shule ya Sekondari ya Dkt. Samia kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, huku akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika elimu kama msingi wa maendeleo ya Taifa.
