Tanzania imeendelea kunufaika na ushirikiano wake na Japan kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo yenye thamani ya mabilioni ya fedha katika sekta za uchumi wa buluu, afya na uimarishaji wa usalama wa baharini.
Akitoa taarifa Bungeni, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Mahmoud Thabit Kombo, amesema kupitia mkutano wa TICAD-9 uliofanyika Yokohama nchini Japan, Tanzania imepata boti za kisasa za doria kwa ajili ya kuimarisha usalama katika Bahari ya Hindi pamoja na miradi ya kuwawezesha wanawake kiuchumi katika maeneo ya mwambao.
Amesema Japan pia imeendelea kufadhili mradi wa ununuzi wa meli ya kwanza ya uvuvi wa bahari kuu inayojulikana kama TAFICO FV.01 pamoja na ujenzi wa kiwanda cha barafu na miundombinu ya kuhifadhi samaki, hatua inayolenga kuongeza thamani ya mazao ya uvuvi.
Katika sekta ya afya, Dkt. Kombo amesema Serikali ya Japan kupitia Tokushukai Medical Corporation imekubali kufadhili ujenzi wa kituo cha umahiri wa matibabu ya figo na upandikizaji katika Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa gharama ya Yen bilioni 1.5.
Amesema miradi hiyo itaimarisha huduma za afya nchini, kupunguza gharama za wananchi kutafuta matibabu nje ya nchi, pamoja na kuchochea ukuaji wa uchumi wa buluu na kuongeza ajira kwa Watanzania.
