Tanzania imeendelea kuimarisha ushirikiano wa kikanda kupitia mikutano mbalimbali ya kimkakati na nchi jirani ikiwemo Rwanda, Uganda, Burundi na Msumbiji, ikiwa ni sehemu ya kukuza maendeleo ya kiuchumi na ushirikiano wa kikanda.
Akitoa taarifa Bungeni, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Mahmoud Thabit Kombo, amesema kupitia Mkutano wa 16 wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Rwanda uliofanyika Kigali, nchi hizo zilifikia makubaliano ya kuimarisha ushirikiano katika sekta za biashara, uchukuzi, uwekezaji na mawasiliano, pamoja na kusaini makubaliano ya ushirikiano katika sekta ya kilimo.
Amesema Tanzania na Uganda zimesaini makubaliano ya maendeleo ya reli ya kisasa ya SGR kutoka Isaka hadi Uganda kupitia mradi wa Isaka–Lusahunga–Murongo hadi Kikagati–Mpondwe, hatua inayolenga kuboresha miundombinu ya usafirishaji na kuongeza ufanisi wa biashara za kikanda.
Kwa upande wa Burundi, Serikali imesema ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Uvinza hadi Musongati yenye urefu wa kilomita 282 unatarajiwa kuchochea biashara na mtangamano wa kikanda utakapokamilika.
Aidha, Wizara hiyo imeeleza kuwa Tanzania na Msumbiji zinaendelea kushirikiana katika masuala ya ulinzi na usalama, hususan katika mapambano dhidi ya ugaidi mpakani, ili kuhakikisha amani na utulivu katika ukanda wa kusini mwa Afrika.
