Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeonya kuhusu kuendelea kwa mvutano wa kisiasa na kiusalama katika ukanda wa Mashariki ya Kati, ikieleza kuwa hali hiyo inaendelea kuathiri uchumi wa dunia pamoja na Tanzania.
Akiwasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara hiyo Bungeni, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Mahmoud Thabit Kombo, amesema mgogoro unaozihusisha Marekani, Israel na Iran umeendelea kuzua taharuki katika siasa za kimataifa na masoko ya uchumi duniani.
Dkt. Kombo amesema chanzo kikuu cha mvutano huo ni mpango wa nyuklia wa Iran, ambapo Marekani na Israel zimekuwa zikihofia Iran kupata uwezo wa kutengeneza silaha za nyuklia, huku Iran ikisisitiza kuwa mpango huo unalenga matumizi ya kawaida ya nishati.
Amesema licha ya kufikiwa kwa makubaliano ya muda ya kusitisha mapigano, hali ya tahadhari bado ipo na tayari imeanza kuathiri uchumi wa mataifa mbalimbali kupitia kupanda kwa bei za mafuta na nishati katika soko la dunia.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, athari hizo zimechangia pia kuongezeka kwa mfumuko wa bei nchini Tanzania kutokana na utegemezi wa soko la kimataifa la mafuta.
Aidha, Dkt. Kombo amesema migogoro ya Israel na Palestina pamoja na hali ya Yemen na Syria bado inaendelea kusababisha madhara makubwa ya kibinadamu ikiwemo uharibifu wa miundombinu, ongezeko la wakimbizi na kudhoofika kwa biashara za kimataifa.
