Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imesema itaendelea kushiriki kikamilifu katika juhudi za kuleta amani na utulivu duniani huku ikiimarisha ushirikiano wake kupitia jumuiya za kikanda na kimataifa.
Akiwasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara hiyo Bungeni, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Mahmoud Thabit Kombo, amesema migogoro inayoendelea katika baadhi ya nchi za Afrika ikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Sudan, Sudan Kusini, Somalia pamoja na Ukanda wa Sahel bado ni changamoto kubwa kwa maendeleo na ustawi wa bara hilo.
Dkt. Kombo amesema Tanzania itaendelea kuunga mkono juhudi za kutafuta suluhisho la migogoro hiyo kupitia mazungumzo ya amani yanayosimamiwa na jumuiya za kikanda na kimataifa ikiwemo Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Afrika (AU) pamoja na Umoja wa Mataifa (UN).
Aidha, amepongeza uteuzi wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Mrisho Kikwete, kuwa Mjumbe Maalum wa Pembe ya Afrika, akieleza kuwa hatua hiyo imeendelea kuipa Tanzania heshima na ushawishi mkubwa katika diplomasia ya kimataifa.
Dkt. Kombo amesema uzoefu mkubwa wa Dkt. Kikwete katika usuluhishi wa migogoro unatarajiwa kusaidia juhudi za kuleta amani na utulivu katika eneo la Horn of Africa ambalo limeendelea kukabiliwa na changamoto za kisiasa na kiusalama kwa muda
