CHINA YAIFUTIA TANZANIA DENI LA BILIONI 34 NA KUONGEZA UFADHILI WA MIRADI YA MAENDELEO


Serikali ya China imeifutia Tanzania deni la zaidi ya Shilingi bilioni 34 lililotokana na mkopo usio na riba uliotumika kujenga Ofisi Ndogo ya Wizara ya Mambo ya Nje jijini Dar es Salaam.

Akitoa taarifa Bungeni, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Mahmoud Thabit Kombo, amesema hatua hiyo ni sehemu ya matokeo ya ziara rasmi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi, aliyefanya ziara nchini Januari 2026.

Amesema pamoja na msamaha huo wa deni, China imeahidi kuendelea kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo kupitia mpango wa FOCAC, ikiwemo miradi ya teknolojia ya malisho ya mifugo, kuboresha huduma za afya pamoja na kupeleka madaktari bingwa wa kujitolea nchini Tanzania.

Aidha, Dkt. Kombo amesema China imeunga mkono rasmi azma ya Tanzania kuwania nafasi ya ujumbe usio wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kipindi cha 2029 hadi 2030.

Amesema hatua hiyo inaonesha kuimarika kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na China na kuchochea zaidi ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo.

Post a Comment

Previous Post Next Post