Shirika la Reli Tanzania (TRC) limesema utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR) unaendelea kwa kasi nchini, huku matarajio yakiwa kuifanya Tanzania kuwa kinara wa mtandao wa reli ya kisasa barani Afrika na miongoni mwa mataifa tano bora duniani.
Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Uendeshaji wa TRC, Focus Sahani, wakati wa uzinduzi wa kampeni ya #NusuMudaKotekote uliofanyika leo Mei 8, 2026 jijini Dar es Salaam.
Amesema baada ya kukamilika kwa kipande cha Dar es Salaam hadi Dodoma, Serikali kupitia TRC inaendelea na ujenzi wa kipande cha Makutupora hadi Tabora pamoja na Tabora hadi Isaka chenye urefu wa kilometa 165.
Aidha amesema ujenzi wa kipande cha Isaka hadi Mwanza chenye kilometa 341 pamoja na reli ya Tabora hadi Kigoma unaendelea ikiwa ni sehemu ya mpango wa kupanua mtandao wa SGR nchini.
“Baada ya kukamilika kwa vipande vya Dar es Salaam hadi Dodoma sasa tunaendelea na ujenzi wa kipande cha Makutupora kwenda Tabora, lakini pia Tabora hadi Isaka, Isaka hadi Mwanza na Tabora hadi Kigoma. Huko kote ujenzi unaendelea,” alisema.
Sahani amesema TRC pia imekamilisha upembuzi yakinifu wa miradi mingine ya reli ikiwemo kipande cha Moshi hadi Arusha, ambapo kutakuwa na reli ya SGR itakayounganisha Tanga, Arusha na Musoma.
Ameongeza kuwa upembuzi yakinifu wa reli ya kutoka Mtwara hadi Mbamba Bay yenye urefu wa kilometa 1,028 pia umekamilika, huku hatua inayofuata ikiwa ni upatikanaji wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.
Kwa mujibu wa Sahani, utekelezaji wa miradi hiyo unalenga kuongeza muunganiko wa usafiri wa reli katika maeneo mbalimbali ya nchi pamoja na kuchochea shughuli za kiuchumi na kijamii.
“Yote hiyo ni kuonesha kwamba eneo kubwa la nchi linapatiwa reli ya kisasa ya SGR,” alisema.
Vilevile amesema kukamilika kwa miradi yote ya SGR kutafanya Tanzania kuwa na takribani kilometa 4,752 za reli ya kisasa, hatua ambayo itaifanya nchi kuwa ya kwanza Afrika kwa ukubwa wa mtandao huo na miongoni mwa nchi tano bora duniani.
“Tutakapokuwa tumemaliza takribani kilometa 4,752 zitakuwa zimetandikwa reli ya SGR. Kwa Afrika tutakuwa tunaongoza na duniani tutakuwa tano bora, ni jambo la kujivunia,” alisema.
Katika hatua nyingine, Focus ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika sekta ya reli na kulipa kipaumbele Shirika la Reli Tanzania huku akisisitiza kuwa, uwekezaji mkubwa unaofanywa katika reli ya kisasa umeendelea kuboresha huduma za usafiri nchini pamoja na kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa watu na mizigo.
Pia amewahimiza wananchi kutumia huduma ya SGR kutokana na usalama, kasi na ubora wake huku akiwataka kulinda miundombinu ya reli kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
“Tutumie usafiri salama na wenye tija wa SGR ambao una kasi ,salama na unarahisisha wananchi kufika mapema kwenye majukumu yao,” alisema.
Aidha amesema watendaji wa TRC wanaendelea kuhakikisha huduma bora zinatolewa kwa wananchi sambamba na kupokea ushauri utakaosaidia kuboresha zaidi huduma za shirika hilo.
