Shirika la Reli Tanzania (TRC) limezindua kampeni maalumu ya #NusuMudaKoteKote ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka miwili tangu kuanza kwa huduma ya usafiri wa reli ya kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR), hatua inayodhihirisha mafanikio ya maboresho ya sekta ya usafiri nchini.
Kampeni hiyo inalenga kuonesha mchango wa SGR katika kurahisisha usafiri, kupunguza muda wa safari pamoja na kuimarisha shughuli za kijamii na kiuchumi kwa wananchi ndani na nje ya Jiji la Dar es Salaam.
Tangu kuanza kwa huduma hiyo Juni 14, 2024, SGR imeendelea kujijengea sifa kwa kutoa usafiri wa kisasa wenye viwango vya kimataifa, huku safari kati ya mikoa mbalimbali zikifanyika kwa muda mfupi zaidi ukilinganisha na ilivyokuwa hapo awali.
Kupitia kampeni hiyo, TRC imeeleza kuwa ndani ya miaka miwili ya uendeshaji, wananchi wengi wameendelea kunufaika na huduma ya usafiri iliyo salama, yenye hadhi, ustaarabu na inayowawezesha abiria kusafiri kwa ufanisi zaidi.
Aidha, SGR imeendelea kuwa chachu ya ukuaji wa shughuli za biashara na uchumi kutokana na uwezo wake wa kurahisisha usafirishaji wa watu na kuongeza muunganiko kati ya maeneo mbalimbali ya nchi.
Kaulimbiu ya “Safiri, Fanya Kazi, Fika Haraka” imetajwa kuakisi dhamira ya huduma hiyo katika kuwapatia wananchi usafiri wa uhakika unaookoa muda na kuongeza tija katika shughuli za kila siku.
Katika maadhimisho hayo, TRC imebainisha kuwa kampeni ya #NusuMudaKoteKote pia inalenga kuhamasisha wananchi wengi zaidi kutumia huduma ya SGR ambayo imeendelea kuwa alama ya maendeleo ya miundombinu ya kisasa nchini.
Huduma ya SGR imeendelea kuvutia makundi mbalimbali ya abiria wakiwemo wafanyabiashara, wanadiplomasia, wanafunzi, watumishi pamoja na wageni kutoka ndani na nje ya nchi kutokana na ubora wa huduma na mazingira rafiki ya usafiri.
Kwa mujibu wa TRC, maadhimisho ya miaka miwili ya SGR yanaashiria hatua muhimu katika historia ya usafiri wa reli nchini huku matarajio yakiwa ni kuendelea kuboresha huduma hiyo ili kukidhi mahitaji ya wananchi wengi zaidi.
