Mdau wa huduma ya usafiri wa Reli ya Kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR) ambaye pia ni Meneja wa Mwanariadha Alphonce Simbu, Bw. Moses Simon amesema ujio wa usafiri huo umeleta mapinduzi makubwa katika sekta ya usafiri nchini na kukifanya kizazi cha sasa, hususan Gen-Z, kushuhudia huduma za kisasa ambazo hapo awali hazikuwepo kwa kiwango hicho.
Simon amezungumza hayo leo Ijumaa Mei 08, 2026 katika uzinduzi wa kampeni ya #NusuMudaKoteKote iliyoandaliwa na Shirika la Reli Tanzania (TRC)
ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka miwili tangu kuanza kwa huduma ya usafiri wa SGR, hatua inayodhihirisha mafanikio ya maboresho ya sekta ya usafiri nchini pamoja kuonesha mafanikio ya SGR katika kupunguza muda wa safari, kuongeza usalama wa abiria na kurahisisha shughuli za kijamii na kiuchumi.
Mdau huyo amesema tofauti kati ya usafiri wa zamani wa reli ya zamani (MGR) na huduma ya sasa ya SGR ni kubwa kutokana na kasi, ubora na ufanisi wa usafiri huo.
Amesema wakati akisoma kidato cha kwanza hadi cha sita mkoani Njombe, safari za treni kutoka Dar es Salaam kwenda Makambako zilikuwa zikichukua zaidi ya siku moja kufika, tofauti na hali ilivyo sasa kupitia reli ya kisasa ya SGR.
“Nimesoma kidato cha kwanza hadi cha sita mkoani Njombe. Unapanda treni ya MGR saa moja asubuhi Dar es Salaam, unafika Makambako kesho yake saa nane au saa tisa jioni. Gen-Z wamekutana na vitu vizuri sana,” alisema.
Ameendelea kwa kusema kuwa usafiri wa treni una mchango mkubwa katika kupunguza gharama za safari huku ukiwapatia abiria mazingira mazuri na uzoefu tofauti wa usafiri ukilinganisha na njia nyingine.
Amesema katika mataifa mengi yaliyoendelea, reli ni moja ya mifumo mikuu ya usafiri wa umma, jambo linalomfanya kuiona SGR kama hatua muhimu ya maendeleo kwa Tanzania.
“Mimi naifurahia SGR kwa sababu katika nchi za wenzetu nikitembelea huu ndio usafiri wangu,” alisema.
Aidha amesema uwepo wa SGR umeongeza ufanisi wa utekelezaji wa shughuli mbalimbali kutokana na uwezo wa wananchi kusafiri na kurejea ndani ya siku moja kwa gharama nafuu.
“Naweza kuwa na kikao Dodoma, nikatoka asubuhi Dar es Salaam, nikafanya kikao mchana na jioni nikarudi Dar es Salaam kwa kutumia gharama ndogo,” alisema.
Ameongeza kuwa maendeleo ya teknolojia duniani yameifanya jamii kuhitaji mifumo ya kisasa ya usafiri inayookoa muda na kuongeza tija katika shughuli za kila siku.
“Dunia imeenda kasi sana, kila kitu ni teknolojia na huwezi kuikwepa. Vijana wengi wanakimbizana na maisha,” alisema.
Pia amesema matumizi ya SGR yanasaidia kupunguza hatari mbalimbali zinazoweza kujitokeza safarini huku yakirahisisha matumizi bora ya muda kwa wananchi.
“Risk (hatari) nyingi unazikwepa ukitumia SGR. Tuhakikishe tunatumia vizuri muda na kupunguza gharama,” alisema.
Akitoa mfano wa matumizi makubwa ya huduma hiyo, amesema asilimia kubwa ya watu walioalikwa hivi karibuni kuhudhuria shughuli za Bunge wametumia usafiri wa SGR kutokana na urahisi na ufanisi wake.
