SERIKALI YAWEKA MIKAKATI THABITI KUWEZESHA HUDUMA ZA MAWASILIANO ZINAFIKA KWA KILA MTANZANIA


Serikali imeendelea kuonesha dhamira ya dhati ya kuhakikisha huduma za mawasiliano zinawafikia wananchi wote kupitia mipango na mikakati iliyoainishwa katika bajeti ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa mwaka wa fedha 2026/27.

Akiwasilisha hotuba hiyo bungeni Dodoma, Waziri Angellah Kairuki amesema kuwa Wizara itaendelea kutekeleza vipaumbele vinane muhimu, ikiwemo kuimarisha upatikanaji wa huduma za mawasiliano vijijini, kukuza biashara mtandao, na kuimarisha usalama wa mtandao.

Katika kuboresha upatikanaji wa huduma hizo, Serikali inaendelea na ujenzi wa minara 636 katika kata 443, ambapo sehemu kubwa ya minara hiyo tayari imekamilika, na mingine inatarajiwa kukamilika ifikapo mwisho wa mwaka 2026. Mradi huu unatarajiwa kuwafikia wananchi takribani milioni 2.5 waliokuwa hawana huduma za uhakika za mawasiliano.

Vilevile, Serikali imeweka mkazo katika kuendeleza uchumi wa kidijitali kwa kuwezesha upatikanaji wa mitaji kwa kampuni changa za TEHAMA, ambapo tayari shilingi bilioni 5 zimetengwa kusaidia ubunifu na maendeleo ya teknolojia nchini.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, mikakati hiyo inaambatana na malengo ya muda wa kati, ikiwemo kuhakikisha angalau asilimia 55 ya Watanzania wanamiliki simu janja ifikapo mwaka 2027 pamoja na kupunguza gharama za huduma za mawasiliano na intaneti.

Hatua hizi zinatarajiwa kufungua fursa mpya za kiuchumi kwa makundi mbalimbali ya jamii, wakiwemo vijana, wanawake na wajasiriamali, na hivyo kuchochea maendeleo jumuishi yanayochagizwa na teknolojia.

Post a Comment

Previous Post Next Post