TANGA YA VIWANDA YAANZIA KOROGWE


Baadhi  ya wakazi wa Kata ya Mkalamo, wilayani Korogwe mkoani Tanga, wamepongeza juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuvutia uwekezaji wa kiwanda kikubwa cha sukari, wakisema hatua hiyo itachochea ajira na kuongeza mzunguko wa fedha katika wilaya hiyo na mkoa kwa ujumla.

Ujenzi wa kiwanda hicho, kinachotajwa kuwa miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati Afrika Mashariki, ni sehemu ya mpango wa serikali wa kuurejesha Mkoa wa Tanga katika hadhi yake ya kuwa kitovu cha viwanda nchini.

Wananchi hao walitoa maoni yao jana, siku moja baada ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Korogwe, ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya William Mwakilema, kutembelea eneo la mradi huo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi waliitaka serikali kuharakisha mchakato wa uthamini na ulipaji fidia ili kumpa nafasi mwekezaji kuanza ujenzi wa kiwanda hicho mapema.

John Mahimbo, mkazi wa eneo hilo, alisema kuchelewa kwa fidia kunachelewesha utekelezaji wa mradi huo muhimu.

“Sisi tunaona kama serikali inachelewa mchakato wa uthamini na ulipaji fidia. Natamani hata leo nilipwe fidia ili mwekezaji aanze kazi na sisi tupate ajira,” alisema.

Kwa upande wake, Mahunda Mohamed alisema mradi huo utakuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kibiashara kwa wananchi wa Korogwe na Mkoa wa Tanga kwa ujumla.

“Hiki siyo tu kiwanda cha Mkalamo au Korogwe, bali ni cha Mkoa mzima wa Tanga. Mkoa huu ulikuwa na viwanda vingi vilivyokufa, sasa tunaishukuru serikali kwa kuvifufua na kuanzisha vipya,” alisema.

Naye Julius Mhando alipinga taarifa zinazosambaa kuwa wananchi wanapinga mradi huo, akisisitiza kuwa jamii ya eneo hilo inaunga mkono uwekezaji huo.

“Sisi ndio tunakitaka kiwanda hiki. Watakaoajiriwa ni sisi na watoto wetu,” alisema.

Kwa upande wake, mfanyabiashara mdogo (mamalishe) Mage Mgaza alisema wananchi wanasubiri kwa hamu kubwa fursa zitakazotokana na uwepo wa kiwanda hicho.

“Hakuna anayepinga kiwanda kijengwe hapa. Wanaopinga ni watu wa mbali wasiojua hali halisi. Sisi tunaoishi huku tunakitaka kiwanda kijengwe mara moja,” alisema.

Kwa mujibu wa taarifa za mradi, ujenzi wa kiwanda hicho ni sehemu ya mkakati wa serikali kuifanya Tanga kuwa mkoa wa kimkakati wa viwanda, huku wananchi wa maeneo yanayozunguka wakitarajiwa kunufaika moja kwa moja kupitia ajira na shughuli za kiuchumi.

Aidha, imeelezwa kuwa si wananchi wote watahamishwa kupisha mradi huo, bali wale watakaoathirika moja kwa moja watalipwa fidia kwa kuzingatia thamani ya soko, kwa uwazi na kwa makubaliano.

Mkoa wa Tanga uliwahi kuwa miongoni mwa mikoa kinara wa viwanda nchini, ukiwa na viwanda vya kuchakata mkonge, chuma cha Nguvumali, mbolea na sabuni ikiwemo Gardenia, hata hivyo vingi vilidorora na kufungwa. Serikali kwa sasa inaendelea na jitihada za kuvifufua pamoja na kuanzisha viwanda vipya.

Post a Comment

Previous Post Next Post