Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, leo amezindua rasmi kampeni ya Tokomeza Matumizi Batili ya Vipimo katika Soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Vipimo Duniani yatakayofanyika tarehe 20 Mei 2026.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mhe. Chalamila amesema matumizi sahihi ya vipimo yana mchango mkubwa katika kulinda haki za walaji, kuimarisha uadilifu wa biashara pamoja na kujenga mazingira ya ushindani wa haki katika shughuli za kiuchumi.
Aidha, ameipongeza Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) kwa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi na wafanyabiashara kuhusu umuhimu wa matumizi sahihi ya vipimo katika biashara na huduma mbalimbali.
Pia, amewataka wafanyabiashara kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za matumizi ya vipimo ili kuondoa udanganyifu unaoweza kusababisha hasara kwa wananchi na kuathiri uchumi wa taifa. Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na WMA kuhakikisha vipimo vinavyotumika nchini vinakuwa sahihi na vinakidhi viwango vinavyotakiwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ufundi Ndgu. Francis Olwero ameeleza kuwa kampeni hiyo inalenga kuongeza uelewa kwa wananchi na wadau wa biashara kuhusu matumizi sahihi ya vipimo pamoja na kuhamasisha uwajibikaji katika biashara kwa manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla.
