SERIKALI KUPANUA MTO MSIMBAZI, KUJENGA MAENEO SALAMA


Mtendaji mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor Seif amesema mradi wa maendeleo wa Bonde la Msimbazi unatarajiwa kuhamisha zaidi ya nyumba 3,000, kupanua na kuongeza kina cha Mto Msimbazi pamoja na kuongeza uwezo wa maeneo ya mafuriko ili kudhibiti athari za mafuriko jijini Dar es Salaam.

Akizungumza leo katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam, Eng. Seif amesema udongo utakaopatikana kutokana na upanuzi wa mto utatumika kutengeneza maeneo salama kwa makazi na biashara pembezoni mwa bonde, ambapo jumla ya hekta 57 zinatarajiwa kupatikana kwa matumizi hayo.

Amesema mradi huo pia unahusisha ujenzi wa Daraja jipya la Jangwani lenye urefu wa mita 390, linalosimamiwa na TANROADS chini ya Wizara ya Ujenzi.

Kwa mujibu wa Eng. Seif, mradi huo pia utaboresha maeneo ya juu ya bonde kwa kuratibu shughuli za kibinadamu na kudhibiti mmomonyoko wa udongo unaochangia kuziba maeneo ya chini na kusababisha mafuriko.

Mradi huo ulianza rasmi Februari mwaka 2023 na unatarajiwa kutekelezwa kwa kipindi cha miaka sita kwa gharama ya dola za Marekani milioni 260.

Fedha hizo zinatokana na mkopo wa masharti nafuu wa Benki ya Dunia wa dola milioni 200, mkopo kutoka Serikali ya Hispania wa dola milioni 30 pamoja na ruzuku ya Serikali ya Uholanzi ya euro milioni 30.

Eng. Seif amesema hadi sasa mradi umeshalipa fidia ya shilingi bilioni 73.69 kwa waathirika 2,551 ili kupisha utekelezaji wa eneo la chini la bonde, huku kundi jingine la waathirika 314 wanaotarajiwa kuathiriwa na ujenzi wa matuta ya maeneo salama likisubiri kukamilika kwa taratibu za uthamini.

Kuhusu Daraja la Jangwani, amesema ujenzi wake ulianza rasmi mwaka 2025 na unatekelezwa na kampuni ya China Communication and Construction Company Limited kwa gharama ya shilingi bilioni 97.1, huku utekelezaji ukiwa umefikia asilimia 34.

Aidha, amesema mchakato wa kumpata mkandarasi wa kazi ya upanuzi wa mto, maeneo ya mafuriko na maeneo salama ya makazi umefikia hatua za mwisho ambapo leo mkataba unasainiwa rasmi.

Kazi hiyo imepewa kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation kwa ubia na China Railway Construction Corporation pamoja na Harbour Channel Engineering Bureau Group Shanghai Engineering Company Limited kwa gharama ya shilingi bilioni 195.66.

Post a Comment

Previous Post Next Post