DC TARIME AWATAKA WANANCHI KUFUATA TARATIBU ZA KIFORODHA KULINDA USALAMA WA NCHI


Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, ametoa wito kwa wananchi wa eneo la Sirari na maeneo ya jirani kuzingatia taratibu za kiforodha na kushiriki kikamilifu katika kulinda usalama wa nchi, hasa katika maeneo ya mipakani.

Akizungumza na maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) walipo mkoani Mara kutekeleza maagizo ya Kamshna Mkuu Yusuph Mwenda  ya Kutoa Eilimu ya Athari za magendo pamoja na elimu ya kodi, Mkuu wa Wilaya ya Tarime  Meja Edward Gowele amesema changamoto ya magendo na ukwepaji wa kodi bado ni kubwa katika wilaya hiyo kutokana na uwepo wa mipaka yenye njia nyingi zisizo rasmi.

Amesema hali hiyo inachangia kupotea kwa mapato ya serikali pamoja na kuhatarisha usalama wa nchi, akisisitiza kuwa ni jukumu la kila mwananchi kushiriki katika kukabiliana na vitendo hivyo.

“Ni muhimu kwa wananchi kuelewa kuwa kulipa kodi ni wajibu wao wa msingi kwa ajili ya maendeleo ya taifa. TRA si maadui, bali ni washirika wa maendeleo,” amesema Meja  Gowele.

Aidha, amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutoa taarifa sahihi kuhusu vitendo vya magendo vinavyofanyika katika maeneo yao.

Aidha, ameiomba TRA kuendelea kutoa elimu kwa wananchi pamoja na kuongeza vituo vya huduma ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za kikodi kwa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla.

Meja Gowele pia amesisitiza kwa TRA  umuhimu wa kuwashirikisha viongozi wa ngazi za msingi na wanasiasa katika kampeni za elimu ya kodi ili kuhakikisha ujumbe unawafikia wananchi wengi zaidi.

Pia amepongeza juhudi za TRA kufika katika eneo hilo, akieleza kuwa elimu hiyo itasaidia kuongeza uelewa wa wananchi, kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kuboresha usalama wa nchi.

Post a Comment

Previous Post Next Post