WAZIRI SHEMDOE: MRADI WA BONDE LA MSIMBAZI NI SULUHISHO LA KUDUMU LA MAFURIKO DAR ES SALAAM


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Profesa Riziki Shemdoe amesema Serikali imeanza hatua muhimu ya utekelezaji wa Mradi wa Uendelezaji wa Bonde la Mto Msimbazi utakaolenga kumaliza changamoto ya muda mrefu ya mafuriko katika Jiji la Dar es Salaam.

Akizungumza leo Jumatatu Aprili 20, 2026 katika hafla ya utiaji saini wa mkataba wa mradi huo iliyofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam, Profesa Shemdoe amesema mradi huo ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali kujenga jiji salama, lenye ustahimilivu na fursa za kiuchumi.

Ameongeza kwa kusema kuwa, utekelezaji wa mradi huo utaokoa maisha ya wananchi wanaoishi katika maeneo hatarishi kwa kuwahamisha na kuwapatia fidia stahiki, sambamba na kufungua maeneo mapya yatakayochochea shughuli za kiuchumi.

“Hatupanui tu mkondo wa mto, bali tunaweka msingi wa mustakabali bora wa jiji letu kwa kulifanya eneo hili kuwa salama na lenye tija kwa uchumi,” alisema Profesa Shemdoe.

Ameendelea kwa kusema kuwa, Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa ufanisi na kukamilika kwa wakati uliopangwa.

Mradi huo pia unahusisha upanuzi na uongezaji kina cha Mto Msimbazi, ujenzi wa daraja jipya la Jangwani lenye urefu wa mita 390, pamoja na ujenzi wa karakana ya mabasi ya mwendokasi katika eneo la Ubungo Maziwa.

Kwa upande wa gharama, mradi unakadiriwa kugharimu dola za Marekani milioni 260, fedha zitakazotokana na mikopo nafuu kutoka Benki ya Dunia na Serikali ya Hispania pamoja na ruzuku kutoka Serikali ya Uholanzi.

Aidha, mkataba wa utekelezaji wa kazi za awali za uboreshaji wa bonde hilo wenye thamani ya shilingi bilioni 195.66 umesainiwa na kampuni ya China Civil Engineering Construction Cooperation kwa ubia na China Railway Construction Cooperation Harbour Channel Engineering Bureau Group Co., Ltd ambapo utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kubadilisha taswira ya Bonde la Msimbazi na kupunguza kwa kiasi kikubwa athari za mafuriko ambazo zimekuwa zikiathiri wakazi wa Dar es Salaam kwa muda mrefu.

Post a Comment

Previous Post Next Post