WAZIRI MHE. ANGELLAH KAIRUKI: SERIKALI KUJENGA USHIRIKIANO IMARA NA SEKTA BINAFSI KUKUZA UCHUMI WA KIDIJITALI


Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angela Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), ameongoza kikao kazi kati ya Wizara na wadau wa sekta binafsi kilichofanyika katika Ofisi za Wizara hiyo zilizopo Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma, Februari 26, 2026.

Kikao hicho kimekusudia kujadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya Sekta ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari nchini, sambamba na kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika kukuza uchumi wa kidijitali.

Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Kairuki amesema kuwa Wizara inaendelea kutekeleza Programu ya Kitaifa ya Anga za Juu, ikiwa ni utekelezaji wa maono ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoyatoa tarehe 8 Februari 2022, kuhusu Serikali kumiliki satelaiti yake kwa ajili ya kutatua changamoto za mawasiliano nchini.

Amesema programu hiyo inalenga kuimarisha uwezo wa Taifa katika matumizi ya Teknolojia za Anga ili kuboresha mawasiliano, kusaidia sekta za uzalishaji, kuimarisha usalama na usimamizi wa rasilimali, pamoja na kufungua fursa mpya za uwekezaji na ubunifu.

“Ni matarajio yetu kuwa kupitia ushirikiano wa Serikali na Sekta Binafsi, programu hii itachangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza uchumi wa kidijitali na maendeleo ya Taifa kwa ujumla,” amesema Waziri Mhe. Kairuki.

Aidha, Waziri Kairuki ameeleza kuwa Wizara inaendelea kuimarisha Ulinzi wa Miundombinu Muhimu ya TEHAMA (Critical Information Infrastructure – CII) kwa kuzingatia Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 na miongozo mbalimbali ya kutambua, kusajili na kulinda miundombinu hiyo.

Post a Comment

Previous Post Next Post