Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kilimanjaro, Bw. James Jilala, amewakaribisha Watanzania kushiriki katika mbio za Kilimanjaro Marathon zinazotarajiwa kufanyika Jumapili mkoani humo.
Bw. Jilala amebainisha hayo leo Tarehe 21/ 3/ 2026 katika kuelekea maandalizi ya tukio hilo kubwa la kila mwaka, ambapo amesema Mkoa wa Kilimanjaro unaendelea kuwa kitovu cha matukio mbalimbali ya kijamii na kiuchumi, huku Kilimanjaro Marathon ikiwa ni miongoni mwa matukio yanayovutia wadau wengi kutoka ndani na nje ya nchi.
Amesema TRA itashiriki kikamilifu katika tukio hilo kwa kutoa elimu ya kodi kwa wananchi kwa wadau watakaohudhuria.
Ameeleza kuwa kutakuwa na mabanda mawili ya TRA katika eneo la Chuo cha Ushirika, ambapo maafisa wa mamlaka hiyo watakuwepo kutoa huduma na elimu kuhusu masuala ya kodi.
“Nichukue fursa hii kuwakaribisha wadau wote kushiriki nasi katika siku hii muhimu. Tutakutana na wadau mbalimbali na kama TRA tutatumia nafasi hiyo kutoa elimu ya kodi pamoja na huduma mbalimbali,” amesema Jilala.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wananchi na TRA, akiwataka wananchi kudai risiti halali wanapofanya manunuzi ili kuhakikisha uwazi na ulipaji sahihi wa kodi.
Pia amewakumbusha wafanyabiashara kulipa kodi stahiki kwa mujibu wa sheria.
Bw. Jilala ameongeza kuwa kutokana na Mkoa wa Kilimanjaro kupakana na nchi jirani, ni muhimu kwa wananchi kufuata taratibu sahihi za kibiashara, hususan katika masuala ya mipakani ili kuepuka ukiukwaji wa sheria.
Aidha, amesema mwezi Machi ni kipindi cha makadirio ya kodi, hivyo amewahimiza walipakodi ambao bado hawajafanya makadirio kutumia mfumo wa kisasa wa IDRAS, ambao ni rahisi, rafiki na shirikishi kwa watumiaji.
Meneja huyo amewahakikishia wananchi kuwa TRA itaendelea kutoa huduma bora kwa wananchi na kujenga mahusiano mazuri na walipakoidi
