Ujumbe wa Kampeni ya Kitaifa ya Kuhamasisha Uwekezaji wa Ndani kutoka Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) umewasili leo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi na kueleza malengo matatu ya kampeni hiyo.
Malengo hayo ni kutembelea miradi ya Watanzania ili kuhamasisha wengine kuwekeza, kutoa semina ya elimu ya uwekezaji kwa wakazi wa Katavi, pamoja na kuzindua rasmi Dawati la Uwekezaji mkoani humo ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Mheshimiwa Rais ya kusogeza huduma karibu na wananchi.
Mkuu wa Mkoa, Mhe. Mwanamvua Hoza Mrindoko, amesema TISEZA ina jukumu la kubadili mtazamo hasi wa baadhi ya Watanzania kuhusu uwekezaji. “Tunahitaji kuwa na mamilionea na mabilionea kutoka Katavi,” amesisitiza, akibainisha kuwa mkoa umetenga ekari 521 kwa uwekezaji huku 2,500 zikiwa katika maandalizi.
Fursa zilizopo ni pamoja na kilimo, mifugo, madini, huduma za kijamii na utalii, hususan katika Hifadhi ya Taifa ya Katavi.
Kwa upande wake, Meneja Uhamasishaji Uwekezaji wa TISEZA, Bw. Felix John, amewaalika wakazi wa Katavi kuhudhuria semina itakayofanyika tarehe 27/02/2026 katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
