Ujumbe wa kuhamasisha uwekezaji wa ndani kutoka Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) umetembelea mradi wa Jema Jione Ltd uliopo wilayani Mpanda, mkoani Katavi.
Mradi huo unaojihusisha na uchenjuaji wa madini ya dhahabu na copper na kuzalisha makinikia kwa ajili ya kusafirishwa nje ya nchi, ulisajiliwa TISEZA tarehe 23 Februari 2023. Umewekeza mtaji wa shilingi bilioni moja na kuajiri Watanzania 100. Kwa wastani huzalisha konyena mbili kwa mwezi. Kampuni hiyo pia ina matawi katika Geita, Kahama, Chunya, Muheza na Mvumero.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Meneja wa mradi, Bw. Quintus Kasese, alisema walipata msamaha wa ushuru wa forodha kwa asilimia 75 walipoagiza mitambo ya uzalishaji na malori 40 ya usafirishaji. Alisema msamaha huo uliwawezesha kuokoa gharama na kupanua uwekezaji wao. “Tulipanga kufunga mitambo minne, lakini kutokana na vivutio tulivyopata kupitia TISEZA, sasa tuna mitambo sita,” alieleza.
Kwa upande wake, Meneja Uhamasishaji Uwekezaji wa TISEZA, Bw. Felix John, alimpongeza mwekezaji huyo na kuwahamasisha Watanzania wengine kuthubutu kuwekeza kwa kunufaika na vivutio vinavyotolewa na TISEZA. Aidha, aliwaalika wadau wa uwekezaji mkoani Katavi kuhudhuria semina itakayofanyika kesho katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ili kupata elimu zaidi kuhusu fursa na taratibu za uwekezaji.
