Kanisa Katoliki nchini Tanzania limewasihi waumini wake na Watanzania kwa ujumla bila kujali imani zao, Vyama ama misimamo yao ya kisiasa, kutojihusisha na dhamira yoyote itakayoandaliwa kwa kusudi la kuchochea maandamano, ghasia za machafuko, vurugu au uharibu wa mali za umma na binafsi katika Kipindi cha kuelekea uchaguzi Mkuu wa Tanzania, likihimiza wananchi kushiriki kikamilifu kupiga kura.
Wito huo umetolewa katika Tamko la Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) kuhusu amani kwa Tanzania kuelekea siku ya uchaguzi Mkuu wa Tanzania utakaofanyika Oktoba 29, 2025, Baraza hilo likithibitisha msimamo wake wa dhahiri katika kudumisha amani, umoja na mshikamano wa Tanzania na likisisitiza wajibu wa kila mmoja kuwa kuwa mlinzi wa amani ya Tanzania na kuepuka vitendo vyote vya fujo sambamba na kuheshimu haki na maoni ya watu wengine.
"Kwa kuzingatia historia na uhalisia wa athari za machafuko ya kisiasa ambayo yamekuwa yakishika kasi katika Mataifa mengine ulimwenguni, Kanisa Katoliki linawasihi pia waumini wake na Watanzania kutoshiriki, kuratibu au kuhamasisha mipango ya uvunjifu wa amani ili kulinda ustawi wa Tanzania." Imeongeza Taarifa hiyo iliyoandaliwa na Maaskofu 35 wa Kanisa Katoliki nchini Tanzania na kusainiwa na Rais wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Mhashamu Baba Askofu Wolfgang Pisa na Katibu Mkuu Dkt. Charles Kitima Oktoba 11, 2025.
Baraza hilo la Maaskofu kando ya kujitanabaisha wazi kuwa halijihusishi na masuala ya siasa likiwajibika kutoa mawazo na ushauri wake kwa waumini, limetoa wito pia kwa Kiongozi atakayeshinda katika uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29 kuliongoza Taifa awe tayari kuliunganisha Taifa mara baada ya uchaguzi Mkuu pamoja na kuchukua hatua madhubuti za kuendeleza amani na mshikamano kwa maendeleo ya Taifa la Tanzania na watu wake.
Limesisitiza pia mshikamano wa Kitaifa, heshima ya utu wa mwanadamu na ushirikiano wa kijamii kama nguzo kuu za maendeleo ya Tanzania, wakihimiza Viongozi, waumini na wananchi wote kushirikiana kikamilifu katika kulinda amani, kudumisha umoja wa kitaifa na kuchukua hatua za hekima katika kukabiliana na changamoto za kiuchaguzi kuliko kutumia kauli chonganishi zenye kuweza kuvuruga amani ya Tanzania.