Mgombea Ubunge wa Jimbo la Uyole kupitia Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Tulia Ackson amewataka wananchi wa Mbeya kwa ujumla kummiminia kura za kishindo Mgombea Urais kupitia Chama hicho, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu ili akaikamilishe kazi aliyoianza katika mkoa huo.
Dkt. Tulia ameyasema hayo leo tarehe 12 Oktoba, 2025 wakati akiinadi Ilani ya CCM katika mkutano wa hadhara uliofanyika mtaa wa Gombe kata ya Itezi ambapo amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweza kuboresha sekta mbalimbali hususani katika Jimbo jipya la Uyole ikiwemo miundombinu ya elimu, afya, barabara, maji n.k
Katika hatua hiyo, Dkt. Tulia amebainisha kuwa ili kufanikisha hatua hiyo zaidi basi wananchi hao hawana budi kuipigia kura CCM kuanzia ngazi ya Madiwani, Wabunge pamoja na Rais kwakuwa wamejipanga vyema kuhakikisha wanazitatua changamoto zao kwa kasi isiyoelezeka.
"Tukisalia hapa Jimbo la Uyole, kama tulikuwa na kata 36 kwa Jimbo zima la Mbeya mjini na tukaweza kuleta maendeleo makubwa kiasi hiki na sasa tumegawanywa kwa kuwa na Kata 13 mimi Mbunge wenu wa kujiongeza niwahakikishie tutakimbiza maendeleo kwa kasi ya ajabu hamjawahi kuona" amesisitiza Dkt. Tulia