WAZIRI CHANA AFUNGUA RASMI ONESHO MAALUM LA PICHA LA SERIKALI YA WATU WA CHINA



Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amefungua rasmi onesho maalum la picha katika kuadhimisha miaka 80 ya ushindi wa vita vya upinzani vya watu wa China dhidi ya uvamizi wa Japani na vita vya kupambana na Ufashisti duniani.

Ufunguzi huo umefanyika Agosti 15,2025 katika Makumbusho ya Taifa la Tanzania jijini Dar es Salaam.

 Lengo la onesho hilo ni kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania a Jamhuri ya Watu wa China katika maeneo mbalimbali yakiwemo masuala ya maonesho ya kimakumbusho.

“Tunapotafakari urithi huu wa kihistoria, tunakumbushwa kwamba Tanzania na China zina urafiki wa kina na wa kudumu, unaokita mizizi katika kuheshimiana, mshikamano na matarajio ya pamoja. Tangu siku za mwanzo za uhuru wa Tanzania, ushirikiano wetu umeimarika, ukipanuka katika miundombinu, biashara, elimu, afya, kilimo na kubadilishana utamaduni” amesema Mhe. Chana.

Amefafanua kuwa Oneshi hilo  ni zaidi ya mkusanyiko wa picha na kwamba ni daraja hai kati ya zamani na sasa kwa kuweka kumbukumbu, kuthamini amani, na kubaki thabiti katika azimio kwamba maovu ya vita hayapaswi kurudi tena.

“Tunapopitia maonyesho haya, na tuheshimu urithi wa wale waliopigania uhuru na kuthibitisha dhamira yetu ya pamoja ya kujenga mustakabali unaotokana na amani, ushirikiano na maelewano.”amesema.

Ametumia fursa hiyo kuishukuru Serikali na watu wa China kwa mchango wao wa kudumu katika kuleta amani duniani, na kwa waandaji wa maonyesho hayo kwa kujitolea kwao kuleta historia yenye hadhi na uwazi.

Post a Comment

Previous Post Next Post