GEITA KUANDAA MAANDAMANO KUMSHUKURU RAIS SAMIA UJIO WA MRADI WA TACTIC AWAMU YA PILI.



Mkuu wa Wilaya ya Geita Mkoani Geita Mhe. Hashim Komba ametangaza ujio wa tamasha kubwa na matembezi ya amani kwaajili ya Kumpongeza na kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha ndoto ya wananchi wa Manispaa ya Geita ya kupata kituo kikubwa na cha kisasa cha Mabasi, Kituo ambacho Mkataba wake umesainiwa leo chini ya Mradi wa TACTIC.

Kituo hicho cha mabasi kitakachojengwa kwa fedha Shilingi Bilioni 19, 171, 601,509.00 ni utekelezaji wa awamu ya pili ya Mradi wa TACTIC, ulionuia katika uboreshaji wa miundombinu ya Miji Tanzania, ambapo Mhe. Komba amesisitiza kuendelea kumuombea afya njema Rais Samia ili aweze kutekeleza mageuzi ya kimaendeleo nchini Tanzania.

Akizungumzia matembezi hayo, Mhe. Komba amesema lengo lake litakuwa ni kumtambulisha kwa wananchi Mkandarasi anayetekeleza mradi wa Ujenzi wa Kituo hicho cha mabasi pamoja na barabara za kuingia na kutoka katika kituo hicho sambamba na kuwaonesha wananchi wa Geita muonekana na huduma zitakazopatikana wakati Kituo hicho cha mabasi kitakapokuwa kimekamilika 

"Leo yamekuwa! Kilio kikubwa cha wana Geita ilikuwa ni kupata stendi ya kisasa na hivi karibuni Mwenyenzi Mungu alitupa mtihani wa mvua kubwa kunyesha na eneo ambalo tunalitumia kama Stendi kwasasa lilijaa maji kweli na wote tulichanganyikiwa kwani magari mengine yalielea lakini tunaye Rais ambaye ndani ya muda mfupi ameyafanya yasiyowezekana kufanywa yakafanyika kwa muda mfupi na kwa haraka. Stendi ndani ya wilaya yetu itajengwa,” amebainisha Mhe. Komba.

Katika hatua nyingine Mhe. Komba amebainisha kuwa wajibu wake kama Mkuu wa Wilaya ni kuhakikisha kuwa yaliyomo kwenye Mkataba uliosainiwa leo yanatekelezwa kikamilifu na kwa wakati ili kuhakikisha matokeo na tija  iliyokusudiwa inatimia na wananchi wananufaika na mradi huo mkubwa.

Amewashukuru pia Mkuu wa Mkoa wa Geita pamoja na Baraza la Madiwani la Geita Manispaa kwa ushirikiano wao mkubwa katika hatua za awali za utekelezaji wa mradi huo wa TACTIC akibainisha kuwa Viongozi hao wameweka alama isiyofutika kwa Manispaa ya Geita Mjini.

Post a Comment

Previous Post Next Post