"MIAKA 25 IJAYO MIKOA YA KUSINI IKAENDELEE KUILISHA TANZANIA"- SERUKAMBA


Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe. Peter Joseph Serukamba amesisitiza umuhimu wa wakazi wa mikoa ya Nyanda za Juu kusini kuendelea kutoa maoni yao kwenye uandaaji wa dira mpya ya maendeleo ya mwaka 2050 kutokana na umuhimu mkubwa wa mikoa hiyo katika uzalishaji wa chakula na utoshelevu wa chakula nchini Tanzania.

Mhe. Serukamba aliyewawakilisha wakuu wa mikoa ya Njombe, Mbeya na Songwe ametoa kauli hiyo leo Agosti 03, 2024 Jijini Mbeya, wakati wa kongamano la Kikanda, Kanda ya kusini, la kukusanya maoni ya wananchi kuhusu dira mpya ya maendeleo ya mwaka 2050, ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mhe. Peter Serukamba amesema Mikoa ya nyanda za juu ni vinara katika uzalishaji wa chakula nchini Tanzania na hivyo amewataka wananchi kuja na mawazo na fikra tunduizi zitakazosaidia katika upatikanaji wa dira 2050 itakayowezesha mikoa hiyo kuendelea kuilisha Tanzania kwa miaka 25 ijayo.

Katika hatua nyingine Mhe. Peter Serukamba pia amewashukuru na kuwapongeza viongozi mbalimbali walioongoza Tanzania kwa miaka 25 iliyopita, akisema wamefanikiwa pakubwa kwenye utekelezaji wa dira ya Taifa ya maendeleo ya miaka 25 iliyopita.

Post a Comment

Previous Post Next Post