UMASKINI NA UKOSEFU WA AJIRA KWA VIJANA, CHANGAMOTO KUU UTEKELEZAJI WA DIRA YA TAIFA 2025.


Waziri wa nchi Ofisi ya Rais, Mipango na uwekezaji Mhe. Profesa Kitila Alexander Mkumbo amesema Umaskini pamoja na ukosefu wa ajira kwa Vijana wengi wa Kitanzania ni changamoto kuu zilizoshindwa kutatuliwa kikamilifu kwenye Dira ya maendeleo ya Taifa inayomalizika mwaka 2025/2026.

Mhe. Prof. Kitila Mkumbo amezungumza hayo mapema leo Jumamosi Agosti 03, 2024 kwenye ukumbi wa Eden Highland Jijini Mbeya wakati wa Kongamano la Kikanda, Kanda ya kusini ikiwa ni muendelezo wa utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kukusanya maoni ya wananchi katika uandishi wa dira ya maendeleo ya mwaka 2050.

"Mafanikio ni mengi yaliyotokana na dira ya Taifa ya 2025 lakini changamoto zipo zipo kwani ukuaji wa uchumi haukukua kwa kiwango ambacho kingefanikisha kuondoa umaskini, umaskini bado tunao lakini umepungua." Amesema Prof. Kitila.

Mhe. Waziri wa Mipango na uwekezaji katika hotuba yake amesisitiza wananchi wa mikoa ya Iringa, Mbeya, Songwe na Njombe kutoa maoni yao kikamilifu hasa kwa kuzingatia changamoto hizo za umaskini na ukosefu wa ajira ili kusaidia kupata dira itakayokuwa na suluhu ya changamoto za kiuchumi zenye kuondoa umaskini na kuzalisha ajira nyingi zaidi kwa vijana.

Kufanyika kwa Kongamano hili jijini Mbeya ni muendelezo wa programu maalum inayosimamiwa na Wizara ya uwekezaji na mipango ya kusikiliza wananchi, viongozi wastaafu na waliopo madarakani pamoja na makundi mbalimbali ili kupata maoni yao yatakayojumuishwa kwenye uandishi wa dira ya mwaka 2050.

Post a Comment

Previous Post Next Post