Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amezindua Mwongozo wa utoaji wa elimu ya kujitegemea shuleni ili kuimarisha ujifunzaji na ufundishaji shuleni.
Prof. Mkenda ametoa kauli hiyo mapema leo tarehe 26 Julai, 2024 Jijini Dodoma wakati akizindua Mwongozo wa utoaji wa Elimu ya Kujitegemea katika shule za msingi na sekondari Tanzania Bara na kuitaka jamii kuwajibika katika uchangiaji wa chakula na lishe badala ya kumrudisha nyumbani mwanafunzi au mwanafunzi kutopatiwa chakula awapo shuleni kwa kuwa hajachangia kwani itarudisha nyuma jitihada za kuimarisha ujifunzaji wa mwanafunzi shuleni.
“ni marufuku kwa mwanafunzi yoyote kwenye shule za Umma kurudishwa nyumbani kwa sababu tu mzazi hajachangia mchango wa aina yoyote ukiwemo chakula ambao umekubalika, zipo hatua nyingi zinaweza kuchukuliwa wakati mtoto anasoma” alisema Mhe. Mkenda.
Mkenda amesema katika jamii zetu, vijiji vyetu, kuna ngazi ya utawala na kanuni ambazo zina mamlaka ya kumchukulia hatua mzazi ambaye anagoma kuchangia katika suala la chakula kwa makubaliano yaliyofanyika na wanakijiji na jamii ya shule lakini mwanafunzi asinyimwe chakula kilichochangiwa na wenzake.
Aidha, amempongea Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kusaini Mkataba wa Lishe na Wakuu wa Mikoa kuhusu utekelezaji wa afua za lishe kwani matunda yake yameanza kuonekana kupitia Wakuu wa Mikoa na Wilaya ambao ndio wahamasishaji wa suala la chakula na lishe ikiwemo shuleni kwani ipo mikoa inayofanya vizuri katika kutoa huduma ya chakula ambapo aliitaja mikoa ya Njombe kwa asilimia 98, Kilimanjaro (94), Arusha (88), Pwani (87.8), Iringa (87.2) na Manyara (82.9).
Katika hatua nyingine Prof. Mkenda amesema Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kushirikiana na shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) waliandaa Mpango wa utekelezaji wa Mwongozo wa utoaji wa huduma ya chakula lishe shuleni ambao ulizinduliwa mwezi Novemba, 2023 na utatumiwa na Wadau wa lishe katika kuhamasisha wazazi na walezi kuendelea kuchangia chakula kwa wanafunzi pindi wawapo shuleni.
Akitoa Salamu za mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Sitaki Senyamule amesema mkoa wake umejipanga katika kuhamasisha wazazi kuchangia chakula ili wanafunzi wapate hudma ya chakula na lishe shuleni na kwa sasa ni asilimia 76 ya mashamba na bustani yanalimwa ili kuimarisha utoaji wa chakula katika shule za msingi mkoani humo hii ni sambamba na uzinduzi wa Mpango Mkakati wa ufaulu wa mkoa.
Naye Mwalimu Mkuu shule ya msingi Iyenge Thomas Malembe ameipongeza Global Communities kwa kuwajengea uwezo Kamati ya Shule na Wazazi kwani wazazi waliweza kuchangia kiasi cha shilingi milioni tano ambazo zimesaidia wanafunzi kupata chakula, kuwa na akiba ya gunia 50 za nafaka lakini pia wameweza kuvuna gunia 30 za nafaka na mazao jamii ya kunde zaidi ya kilogramu 500 mwaka 2024 ambazo zimeimarisha suala la chakula na lishe shuleni kuondoa utoro na kuongeza ufaulu.